Satelaiti mbili za Iran zarushwa kwa mafanikio katika anga za mbali + Video
Satelaiti mbili za Iran zilizotengenezwa na wanasayansi wenyewe wa Jamhuri ya Kiislamu mapema leo Jumanne zimerushwa kwa mafanikio angani na kufungua mlango kwa sekta binafsi ya Iran kuingia katika tasnia ya anga za mbali.
Satelaiti za Kowsar na Hodhod zimerushwa kwenye obiti kutokea kituo cha anga za juu cha Vostochny cha mashariki mwa Russia mapema leo Jumanne, kwa kutumia kombora la kurushia satelaiti la Soyuz la Russia.
Mafanikio haya yanaashiria kuingia sekta binafsi ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuzalisha satelaiti na kuzipeleka kwenye anga za mbali. Wataalamu wanasema hiyo ni hatua muhimu na isiyo na kifani katika tasnia ya anga ya juu ya Iran.
Kowsar ni satelaiti yenye nguvu kubwa za kugundua mambo kwa mbali na ina uwezo wa kupiga picha zenye ubora wa hali juu kwa madhumuni mbalimbali katika nyanja tofauti zikiwemo za kilimo, maliasili, mazingira na kudhibiti majanga ya kimaumbile.
Kwa upande wake satelaiti ya Hodhod imeelezwa kuwa ni satelaiti ndogo kidogo yenye programu za mawasiliano, na itakuwa na mchango mkubwa katika Mtandao wa Intaneti (IoT). Miongoni mwa kazi za satelaiti hiyo itakuwa ni pamoja na kutoa huduma za mawasiliano katika maeneo ya mbali na yasiyofikika; maeneo ambayo mitandao ya mawasiliano ya ardhini haipatikani.
Jana Jumatatu, Hassan Salarieh, Mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran alisema kuwa, kufunguliwa njia za anga za juu ni maendeleo ya pili ya aina yake tangu mwezi Machi mwaka jana baada ya Iran kufanikiwa kuweka satelaiti yake ya Chamran kwenye obiti kwa kutumia kombora lake la Qa'em.