Hamas: Kutambuana kati ya "Israel" na "Somaliland" ni mfano hatari
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i134800-hamas_kutambuana_kati_ya_israel_na_somaliland_ni_mfano_hatari
Harakati ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina (Hamas) imetangaza leo Jumamosi upinzani wake dhidi ya tangazo la utawala uliojitenga na Somalia katika eneo la "Somaliland" la kutambuana rasmi na Tel Aviv, ikisisitiza kuwa hatua hiyo "ni mfano hatari na jaribio lililoshindwa la kupata uhalali bandia dola vamizi linalohusika katika uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari."
(last modified 2025-12-27T12:11:01+00:00 )
Dec 27, 2025 12:11 UTC
  • Hamas yapinga hatua ya Israel na Somaliland ya kutambuana rasmi
    Hamas yapinga hatua ya Israel na Somaliland ya kutambuana rasmi

Harakati ya Kiislamu ya kupigania ukombozi wa Palestina (Hamas) imetangaza leo Jumamosi upinzani wake dhidi ya tangazo la utawala uliojitenga na Somalia katika eneo la "Somaliland" la kutambuana rasmi na Tel Aviv, ikisisitiza kuwa hatua hiyo "ni mfano hatari na jaribio lililoshindwa la kupata uhalali bandia dola vamizi linalohusika katika uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari."

Taarifa ya Hamas imesisitiza upinzani wake mkubwa dhidi ya mipango ya utawala vamizi wa Israel ya kuwahamisha kwa mabavu watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na mapendekezo yanayozungumzia kutumia "Somaliland" kama ardhi mbadala kwa ajili ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Hamas imeeleza kwamba hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutambua rasmi utawala wa Somaliland uliojitenga na Somalia inaonyesha kina cha kutengwa kimataifa kunakoisumbua Israel kutokana na uhalifu wa mauaji ya limbari uliyoyafanya huko Gaza. Hamas imetoa wito wa kuimarishwa kutengwa huko katika ngazi mbalimbali, na kufanya kazi ya kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa uhalifu wao dhidi ya ubinadamu.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema Ijumaa kwamba Tel Aviv imetambua rasmi Somaliland kama “taifa huru na lenye mamlaka kamili” na kusaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo.

Netanyahu alihusisha uamuzi huo na “Mkataba wa Abraham” ulioanzishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika urais wake wa kwanza, akisema ndio msingi wa kutambua rasmi Somaliland.

Jana Ijumaa Umoja wa Afrika (AU) ulipinga vikali jaribio lolote la kutambua eneo lililojitenga la Somaliland kama taifa huru, ukisisitiza tena dhamira yake thabiti ya kulinda umoja, mamlaka na mipaka ya ardhi ya Somalia.

Vilevile, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (P-GCC) pia zimelaani hatua ya Israel, zikisema ni “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na uvunjaji wa wazi wa kanuni za umoja na mamlaka ya mataifa.”