Juhudi za Iran na Serbia za kupanua ushirikiano wa kiuchumi baina yao
Rais wa Jamhuri ya Iran amesema katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Serbia kwamba, uhusiano wa nchi hizo mbili hususan katika nyanja za kiuchumi na kibiashara unahitaji kuboreshwa na kustawishwa zaidi.
Seyyid Ebrahim Rais alisema Jumapili ya 23 Julai, katika mazungumzo yake na Vladimir Orlić, Spika wa Bunge la Serbia na kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono amani, uthabiti na utulivu wa eneo la Balkan na kwamba, Iran haioni kama kuna kizingiti katika kupanua ushirikiano na mataifa ya eneo hilo. Ebrahim Raisi amesisitiza pia kwamba, kuna ulazima wa kutambua uwezo na fursa zilizopo na wakati huo huo kuainishwa njia na mikakati ya kustawishwa uhusiano katika Kamisheni ya Pamoja ya nchi mbili za Iran na Serbia.
Uhusiano wa Iran na Serbia, ikiwa ni turathi kuu wa Yugoslavia ambayo ni mmoja wa waasisi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), ni mkongwe na wa muda mrefu, na historia ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili inapaswa kutambuliwa kuwa hauna nukta hasi.
Serbia ikiwa ni mwanachama mwangalizi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, ina uhusiano na ushirikiano mzuri na nchi wanachama wa harakati hii ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi hizo mbili zimekuwa zikitaka kupanua uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali hususan za kiutamaduni na kiuchumi katika muongo mmoja uliopita.
Safari za maafisa wa Iran na Serbia kati ya Tehran na Belgrade zimeongezeka katika miaka michache iliyopita, ikiwa ni pamoja na safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wa Serbia mjini Tehran mwezi Aprili 2021 na safari ya Hussein Amir- Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Belgrade na kukutana na Rais na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serbia mwezi Disemba 2022. Pia, mwezi Mei 2022, Marais wa Jamhuri ya Iran na Serbia walifanya mazungumzo kwa njia ya simu ambapo walitoa mwito wa kuongezwa maingiliano na kupanuliwa kiwango cha uhusiano kati ya Tehran na Belgrade.
Hata hivyo, licha ya uwezo wa kiuchumi wa Iran na nafasi nzuri ya Serbia barani Ulaya, lakini kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya pande hizo mbili hakijaongezeka na kuwa katika kiwango sawa na uhusiano mzuri wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili; na kipindi fulani kutokana na vikwazo na kuenea kwa virusi vya Corona, kilichukua mkondo wa kupungua. Kwa mfano, mwaka wa 2020, Iran ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola milioni 16 kupeleka Serbia, na taifa hilo liliingiza nchini Iran bidhaa za thamani ya dola milioni 7. Hii ni katika hali ambayo, kiwango uhusiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili kilikuwa kimefikia thamani ya dola milioni 200 mwaka 2018.
Pamoja na hayo, dhamira ya nchi mbili hizi ya kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi, kwa mara nyingine tena imepanua mwelekeo wa uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Serbia, na kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Biashara la Jamhuri ya Serbia, thamani jumla ya mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili na thamani ya mauzo ya Iran kwa Serbia iliongezeka mwaka 2021 ikilinganishwa na 2020.
Wakati huo huo, mkutano wa Tume ya Pamoja ya Uchumi ya Iran na Serbia umepangwa kufanyika Tehran mwezi Oktoba au Novemba mwaka huu (2023) sambamba na safari ya ujumbe wa wafanyabiashara wa Serbia hapa Iran. Katika mikutano hii, kutajadiliwa vizingiti vya ushirikiano wa kibiashara, hasa katika nyanja ya miamala ya benki na masuala ya forodha, na maafisa husika watajadili na kubadilisha mawazo kuhusu njia na mbinu mbadala na za lazima kwa minajili ya kuondoa vizingiti katika njia hiyo.
Ni dhahir shahir kwamba, uwezo wa nchi hizo mbili ni mkubwa katika nyuga mbalimbali zikiwemo za kilimo, utalii na viwanda, na irada na azma ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Serbia pia ni kuimarisha ushirikiano hususan katika uga wa kiuchumi. Kwa muktadha huo, safari ya Spika wa Bunge la Serbia mjini Tehran inaweza kutathminiwa kwamba, lengo lake ni kuimarisha ushirikiano wa Kibunge na hivyo kusukuma mbele na kwa haraka gurudumu la ushirikiano wa mataifa haya mawili.
Spika wa Bunge la Serbia, sambamba na kusisitiza hamu na shauku ya nchi yake ya kustawisha na kuzidisha kiwango cha uhusiano wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika sekta ya viwanda na kilimo amesema: "Hatuko tayari kuongeza kiwango cha ushirikiano tu, bali pia tunafanya juhudi ili kufikia lengo hili, na kuwa na kamisheni ya pamoja kati ya nchi hizi mbili bila shaka kutakuwa na ufanisi katika kuimarisha na kupanua uhusiano hasa katika uga wa kiuchumi.