Mpango wa Marekani: Kuanzisha mgogoro nchini Iran
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, Marekani ilichukua nafasi ya kiongozi wa kambi ya Magharibi ambayo siku zote imekuwa ikijaribu kuchukua nafasi ya hegemonia (mamlaka ya kutoa amri) katika eneo la Asia Magharibi.
Tangu wakati huo Marekani imechukua mkondo wa chuki dhidi ya Iran. Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Marekani imekuwa ikitekeleza sera na hatua za upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa njia mbalimbali, kama vile kuweka vikwazo vya kiwango cha juu kabisa, vitisho vya kijeshi, kuanzisha kampeni za kisiasa na kidiplomasia na vita vya kisaikolojia.
Licha ya kutokuwa na tija kwa sera na hatua za upande mmoja za Marekani dhidi ya Iran, lakini Washington bado inasisitiza juu ya kuendelezwa mbinu hiyo haramu dhidi ya Tehran ambayo kimsingi ni kinyume na mkataba wa Umoja wa Mataifa. Katika kipindi cha utawala wa Urais wa Joe Biden, naye alianzisha vita mseto (vita jumuishi) dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akitumia visingizio mbalimbali.
Miongoni mwa hatua za Marekani dhidi ya Iran ni jaribio la kuanzisha na kuchochea machafuko nchini Iran, kwa upande mmoja, kwa kudai kuwa inawaunga mkono wananchi wa Iran hususan wanawake na kuhimiza na kuunga mkono makundi yanayotaka kujitenga nchini Iran. Mfano wa wazi wa hili ni uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na washirika wake wa Ulaya kwa machafuko ya 2022 nchini Iran.
Viongozi wa Marekani wamekuwa wakizungumza mara kwa mara kuhusu haja ya kuigawa Iran. Lengo lao ni kuupindua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaotawala hapa nchini na kuigawanya nchi hii yenye historia ya miaka elfu kadhaa ya ustaarabu, na kuifanya igawike sehemu kadhaa kwa vigezo vya ukaumu ili kwa njia hiyo kama wanavyoota ndoto za alinacha waufute mfumo wa Kiislamu, ambao ni mmoja wa wapingaji wakubwa wa sera za kibabe na kiburi za Marekani katika eneo.
Kwa mara ya kwanza baada ya Vita vya Pili vya Dunia, James Byrnes, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani wa wakati huo alichora ramani na kuigawa Iran katika sehemu 7 kulingana na kaumu zake. Wakati huo, James Byrnes alidhani kuwa Iran sio nchi muhimu katika milinganyo ya siasa za ulimwengu, kwa hivyo aliwasilisha mpango wa kuigawa Iran katika nchi 7 ndogo.
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu, njama za Marekani za kuigawa Iran kwa kutumia tofauti za kikaumu na kidini zilikuwa kwenye ajenda tena. Mpango wa "Mashariki Kubwa ya Kati" wa Bernard Lewis, mhadhiri wa Chuo Kikuu, pia anasisitiza mgawanyo wa nchi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Lewis anasema: "Nchi za Kiislamu ni tishio kwa ulimwengu wa Magharibi, na nchi hizi lazima zigawanywe ili kudhoofisha nguvu ya Uislamu mara moja na kwa daima; vinginevyo Uislamu utaangamiza Magharibi."
Lakini kitovu kikuu na sehemu cha mpango wake ilikuwa kuigawa Iran: Kulingana na mpango wa Lewis, Iran itagawanywa katika sehemu 6. Kwa hakika, sehemu za Iran zitaungana na nchi jirani, na makabila ya Baloch, Kiarabu, Kituruki, na Kikurdi yatajitenga na Iran.
Kwa njia hiyo, Marekani ikiwa ni shetani mkubwa na adui mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima inataka kutekeleza mpango wake wa kiuadui wa kuigawa Iran na katika suala hili, Washington ina mipango kadhaa inaitazama kkama fursa ya kuzusha migogoro nchini Iran kama vile kuanzisha na kuchochea tofauti za kikabila na kidini, kuibua migogoro ya kijinsia kwa kudai kuunga mkono wanawake wa Iran na haki zao, jambo ambalo lilitiliwa mkazo zaidi katika ghasia na machafuko ya 2022.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza mara kwa mara kuhusiana na njama za Marekani katika uga wa kuzusha mgogoro nchini Iran na nchi nyinginezo.
Jumatatu ya juzi tarehe 11 Septemba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alionana na wananchi wa mikoa miwili ya "Sistan na Baluchistan" na ule wa "Khorasan Kusini" ambapo sambamba na kubainisha kwamba, dunia ya leo iko ukingoni mwa mabadiliko makubwa alisema: Kuvuruga umoja wa kitaifa na kudhoofisha usalama wa taifa hili, ni malengo makuu ya maadui wa Iran lakini na sisi tumesimama imara na hatutetereki katika kukabiliana na adui. Tuna yakini kwamba maadui wa Iran yetu azizi hawawezi kufanya upuuzi wowote iwapo wananchi na viongozi wao wataendelea kuwa macho na kutoghafilika.
Aidha alisema: Wao wamefikiri na kufanya utafiti na kufikia natija kwamba, kuna nukta kadhaa za kuzusha migogoro nchini Iran: Tofauti za kikabila, tofauti za kimadhehebu, na suala la jinsia na kadhia ya mwanamke ambayo haya yanapaswa kutumiwa kwa ajili ya kuanzisha mgogoro. Huu ni mpango wa Marekani.
Sisitizo la Ayatullah Khamenei juu ya kutokuwa na tija kwa njama za Marekani za kuzusha mzozo dhidi ya Iran, ambazo zilianzia katika kujaribu kuweka vikwazo vya kila upande na kufanya njama za kuzusha mgogoro na kujaribu kuibua machafuko na kuyachochea, na kutumia makabila na wanawake kama nyenzo linaonyesha kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ambao daima umekuwa ukiegemea uungaji mkono wa wananchi pamoja na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, una mizizi na nguvu zaidi na hivyo hauwezi kushindwa na uadui na njama za Marekani na washirika wake.