Kutumia vibaya nchi za Magharibi Mashirika ya Kimataifa kuishinikiza Iran
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kukosoa siasa za nchi za Magharibi amesema, nchi hizo zinatumia vibaya chombo hicho kama silaha ya kuishinikiza Iran.
Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) wamekutana kando ya mkutano wa kila mwaka wa 67 wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na kujadiliana kuhusiana na suala la kuimarisha ushirikiano wa kiufundi kati ya Iran na wakala huo pamoja na kuboresha uhusiano wa pande mbili.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI) ameashiria katika kikao hicho kushindwa siasa za kidhalimu za nchi za Magharibi dhidi ya Iran na kuongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitanyamaza kimya na itatoa jibu muafaka kwa mashinikizo yoyote ya kisiasa dhidi yake.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuja baada ya Rafael Grossi IAEA kurudia madai yake ya kisiasa kuhusu makubaliano ya kiusalama na Iran chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), na kusisitiza juu ya ulazima wa kutatuliwa na kupitishwa masuala yaliyobakia, baada ya kupita miaka kadhaa. Grossi aidha amedai kuwa haridhishwi na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano ya mwezi Machi na Iran.
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran mnamo Machi 1401 na kufuatia ziara ya siku mbili ya Rafael Grossi mjini Tehran, walifikia makubaliano kuhusiana na utatuzi wa madai ya kisiasa yanayotolewa dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ambapo Iran ilikubali kutoa kibali kwa shirika hilo wa kukagua vituo vyake vya nyuklia. Suala ambalo lingetekelezwa na kufuatiliwa kwa karibu zaidi kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Majilisi ya Ushauri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (sheria ya hatua ya kimkakati ya kufuta vikwazo na kulinda maslahi ya taifa la Iran).
Licha ya ushirikiano endelevu wa Iran, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unapuuza ushirikiano mzuri na wa kujitolea wa Iran na kuendeleza siasa zake za kundumakuwili na wakati huohuo kuongeza mashinizo dhidi ya Iran. Jambo ambalo linaonyesha kuathiriwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo na siasa za uongo na kujitanua za utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi.
Kuhusiana na hilo, hivi karibuni nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kwa uungaji mkono wa Marekani zilitoa tamko na kurudia madai ya mara kwa mara na yasiyo na msingi dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, suala ambalo lilikabiliwa na radiamali kali ya Iran. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Nasser Kanani amesema: Kwa bahati mbaya, licha ya ushirikiano mzuri na wenye maelewano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakala huo, nchi tatu za Ulaya na Marekani zinatumia vibaya nafasi na ushawishi wao katika wakala huo ili kuharibu anga nzuri ya maelewano na ushirikiano uliopo kati ya Tehran na wakala huo.
Ukweli ni kwamba makubaliano ya nchi wanachama wa AIEA kwa mujibu wa sheria za wakala huo ni tofauti na ahadi zilizotolewa kwa hiari na nchi kama vile Iran. Pamoja na hayo, licha ya Marekani kujitoa katika mapatano ya JCPOA kinyume cha sheria na kuendeleza vikwazo dhidi ya Tehran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kwa hiari kuendelea kutekeleza mapatano ya JCPOA. Kwa msingi huo, kukariri kariri madai yasiyo na msingi katika uwanja dhidi ya Iran na kuyahusisha na makubaliano ya CSA sio tu ni jambo lisilokubalika, bali kunaonyesha malengo ya kisiasa ya nchi za Magharibi na kutumia kwao vibaya wakala huo kutoa mashinikizo dhidi ya Iran.
Ni dhahiri kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kupinga madai hayo, imekuwa ikisisitiza kuwa majukumu ya nchi wanachama wa IAEA kuhusu mapatano ya JCPOA hayataendelea milele bila upande wa pili kutekeleza ahadi zao. Kwa hivyo kama alivyobainisha Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Tehran inatarajia kuwa wakala huo utakuwa ukitoa ripoti zake kwa msingi wa kitaalamu na kiufundi bila kuegemea upanda wowote kisiasa. Hii ni kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya ukaguzi uliofanywa na wakala huo katika vituo na mpango wake mzima wa amani wa nyuklia, ina historia nzuri ya ushirikiano na wakala huo katika uwanja huo, hivyo unapasa kufunga kabisa faili lake la 'masuala yaliyosalia.'