Mtazamo wa kiongozi Muadhamu: Unapodhulumu, subiri kimbunga
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amezungumzia kushindwa "kusikoweza kukarabatiwa" kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa ya vijana wa Kipalestina.
Amesisitiza kuwa: Sababu ya kimbunga hicho kikubwa na haribifu cha vijana hao ni dhulma, uhalifu na umwagaji damu unaoendelea kufanywa utawala huo bandia na ghasibu dhidi ya wananchi wa Palestina, na kwamba utawala huo hauwezi kuendelea kuficha uso na wake wa kutisha na wa kishetani katika kushambulia Ukanda wa Gaza na kuua watu wake kwa kusema uongo na kujidhihirisha kuwa ni mdhulumiwa.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu, ameyasema hayo mapema leo Jumanne katika mahafali ya pamoja ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi, akijibu bwabwaja za baadhi ya maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake, na madai ya kuhusika watu wasio Wapalestina, ikiwemo Iran, katika matukio ya hivi karibuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Amesitiza kuwa: "Hapana shaka kwamba tunabusu vipaji vya nyuso na mikono ya vijana na wabunifu weledi wa Kipalestina, na tunajivunia kwa vijana hao, lakini bwabwaja hizo sio sahihi na mahesabu hayo pia sio sahihi; na wale wanaodai kuwa pigo la hivi karibuni la Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel limetekelezwa na wasio Wapalestina, hawajalifahamu taifa kubwa la Palestina."
Baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, iliyoanzishwa na wanamuqawama wa Palestina chini ya uongozi wa harakati ya Hamas hapo tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba iliyovunja haiba ya utawala wa Kizayuni, baadhi ya duru za Magharibi na za Kizayuni zinajaribu kufidia na kuficha kushindwa huko kukubwa kwa vyombo vya ujasusi na usalama vya Israel na washirika wake kwa kukuza nafasi ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa makundi ya muqawama na athari zake katika operesheni hiyo ya Wapalestina.
Kwa mfano tu, baadhi ya maseneta wa Marekani kama vile Lindsey Graham na Ted Cruz wamedai kuwa, Iran ndiyo iliyohusika na shambulio hilo. Vilevile gazeti la Wall Street Journal limedai kuwa Iran ndiyo iliyoendesha operesheni hiyo kutokea nyuma ya pazia kwa kutuma silaha na kubuni shambulizi kama hilo.
Madai hayo yametolewa wakati serikali ya kidemokrati ya Marekani imetangaza kuwa, hakuna ushahidi wa kuhusika Iran katika operesheni iliyofanywa na Hamas. Kuhusiana na suala hilo, Adrienne Watson, msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya White House amesema: "Fedha zilizoachiliwa za Iran hazina uhusiano wowote na mashambulizi ya Wapalestina huko Israel."
Ukweli ni kwamba, uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa haki halali ya watu wa Palestina ya kujilinda na kukomboa ardhi yao kutoka kwenye makucha ya utawala wavamizi na ghasibu wa Israel umekuwepo kwa muda mrefu na unaendelea. Hali inayoukabili utawala wa Kizayuni wa Israel kwa sasa ni kuongezeka nguvu na irada ya wapigania ukombozi wa Palestina ambayo imepanuka zaidi sio tu katika Ukanda wa Ghaza bali pia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa msingi huo, bwabwaja na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Iran na eti nafasi yake katika Operesheni ya aina yake ya Kimbunga cha al-Aqsa ni jaribio lenye malengo tofauti ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuhalalisha kushindwa kukubwa kwa utawala wa Kizayuni mbele vipigo vya wapigania uhuru wa Palestina. Lengo jingine ni kuudhihirisha utawala huo kuwa umedhulumiwa ili kudumisha himaya na misaada ya Wamagharibi kwa maghasibu hao dhidi ya watu wa Palestina.
Katika hotuba yake ya leo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuunasibisha ushujaa, mbinu na umahiri wa vijana wa Kipalestina kwa watu wasio Wapalestina kupitia madai na bwabwaja kama hizo na kusisitiza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya Jumamosi tarehe 7 Oktoba, siku ya ushujaa wa vijana wa Kipalestina, sio utawala wa Kizayuni wa kabla ya siku hiyo.. Sababu ya balaa hilo kubwa ni matendo ya Wazayuni wenyewe; Kwa sababu unapozidi kikomo katika unyama na ukatili, lazima usubiri "kimbunga".