Safari ya kieneo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye amezitembelea nchi nne za Kiarabu za eneo la Asia Magharibi akiongoza ujumbe wa kisiasa kufuatia matukio ya hivi karibuni ya Palestina, amerejea mjini Tehran baada ya kushauriana na viongozi wa nchi hizo na vilevile baadhi ya viongozi wa harakati za mapambano ya ukumbozi wa Palestina.
Kushindwa vibaya utawala wa Kizayuni dhidi ya makundi ya muqawama wa Palestina katika operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, kumepelekea viongozi wa utawala huo kuwashambulia kinyama raia wa Ukanda wa Gaza kupitia hujuma ya anga na pia kulizingira eneo hilo. Kwa sababu hiyo, Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya safari ya kieneo katika nchi za Iraq, Lebanon, Syria na Qatar ili kushauriana na viongozi wa nchi hizo kuhusu njia za kuzuia kuendelea jinai za utawala huo dhidi ya raia hao wasio na hatia.
Safari ya Amir Abdallahian imeanzia Iraq ambako amejadiliana na Mshauri wa Usalama wa Taifa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo huko Baghdad kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio ya Palestina, na kisha kuelekea Beirut ambako amekutana na kubadilishana mawazo na Waziri Mkuu wa Lebanon, Waziri wa Mambo ya Nje, Spika wa Bunge na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah. Baada ya hapo ameenda Damascus na kukutana na Rais Bashar al-Assad na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Maqdad katika saa chache alizokuwa katika mji mkuu huo.
Baada ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alirejea Beirut na katika hatua ya nne ya safari yake ya kieneo akaenda Doha, mji mkuu wa Qatar, ambapo amejadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya Palestina na Waziri wa Mambo ya Nje na vilevile Amir wa nchi hiyo pamoja na Ismail Haniyah, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas.
Amir Abdollahian aliwaambia waandishi wa habari mjini Beirut siku ya Jumamosi kuwa Iran inaendelea kuchukua hatua zote muhimu za kidiplomasia kwa ajili ya kukomesha jinai na kuondoa mzingiro wa Gaza kupitia mashauriano ya kisiasa na vikao muhimu vya kidiplomasia katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje au wakuu wa nchi za eneo. Amesema, leo Wazayuni wako katika hali mbaya sana na kwamba operesheni ya ushindi na ya kipekee ya Kimbunga cha al-Aqsa kwa mara nyingine tena imethibitisha wazi suala hilo.
Wakati huo huo, utanuaji misuli ya kijeshi wa utawala wa Kizayuni kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza na onyo la kuwalazimisha wakazi wa kaskazini mwa ukanda huo kuhama eneo hilo unaashiria uwezekano wa kuanza operesheni za nchi kavu za Wazayuni katika eneo hilo. Hata hivyo utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu hadi sasa una sababu kadhaa za kuchelewesha operesheni ya nchi kavu dhidi ya Ukanda wa Gaza ikiwa ni pamoja na hofu ya kukabiliwa na majibu makali ya vikosi vya muqawama.
Kile kinachosisitizwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba, iwapo utawala wa Kizayuni utafanya mashambulizi makubwa ya nchi kavu katika Ukanda wa Gaza, kuna uwezekano mkubwa wa kutolewa majibu na vipigo kadhaa kutoka vikosi vya muqawama na kufunguliwa pande mpya za vita katika mgogoro huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Leo viongozi wa makundi ya muqawama wameshikamana, wamezingatia hali zote na wako tayari kufyatua risasi."
Matamshi ya Amir Abdollahian kuhusu onyo la muqawama kwa utawala wa Kizayuni iwapo utaendeleza jinai zake huko Gaza yanaonyesha azma ya mhimili wa mapambano, ya kulipiza kisasi na kusimamisha uchokozi wa utawala huo unaokalia kwa mabavu Beitul Muqaddas.
Nukta nyingine muhimu kuhusu safari ya kieneo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni juhudi zinazofanywa kwa shabaha ya kuziunganisha nchi za Kiislamu na kuzifanya zizingatie zaidi suala la Palestina. Hivi sasa wananchi wa Palestina ndio walengwa wakuu wa mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni, na hadi sasa maelfu ya watu hao wameuawa shahidi au kujeruhiwa. Pia kuna hatari ya kupanuka wigo wa vita, hivyo uungaji mkono wa kivitendo wa nchi za Kiislamu kwa Wapalestina ni muhimu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aidha huku akiashiria ulazima wa kushirikiana pamoja nchi za Kiislamu ili kukomesha jinai za kivita za utawala huo wa kibaguzi dhidi ya raia wa Gaza, amesisitiza umuhimu wa kufanyika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu katika kiwango cha mawaziri wa mambo ya nje na wakuu wa nchi hizo.