Mar 28, 2024 02:18 UTC

Zaidi ya Wairani 100,000 wamehudhuria sherehe kubwa ya kidini katika uwanja wa michezo wa Azadi ambapo kati ya mambo mengine wamewaenzi mashahidi Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hafla hiyo kubwa imefanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam wa Pili wa Waislamu, Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib (AS), ambapo washiriki walionyesha uungaji mkono wao usioyumba kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hafla hiyo iliyofanyika siku ya Jumanne, iliwakutanisha pamoja maelfu ya wapenzi wa Qur'ani, pamoja na wataalamu wa kipindi maarufu cha televisheni cha "Mahfel".

Washiriki walionekana wakiwa wamebeba nakala za Qur'ani Tukufu na bendera za Palestina huku wakisisitiza kuwa kadhia ya Palestina ni kadhia muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hadhirina walisema kuwa hali ya Wapalestina inaumiza nyoyo za Waislamu kote duniani na hivyo mkusanyiko huo ulilenga kuonysha mshikamano na Wapalestina. Wairani, katika mjumuiko huo mkubwa na wa aina yake, walilaani vikali jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Hafla hiyo ya Qur'ani ilihutubiwa na kiongozi wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Ziyad al-Nakhalah, ambaye aliwapongeza wananchi wa Iran kwa uungaji mkono wao usioyumba kwa harakati za ukombozi wa Palestina. Aidha amesema nyoyo za Wapalestina daima ziko pamoja na Wairani kwani Qur'ani tukufu ndiyo inayowaunganisha watu wa mataifa haya mawili. Amesema Wapalestina wataendeleza mapambano yao hadi upatikane ushindi.