Wanachama wa BRICS wameamua kufuta sarafu ya dola katika miamala ya kibiashara
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111930-wanachama_wa_brics_wameamua_kufuta_sarafu_ya_dola_katika_miamala_ya_kibiashara
Iran imesema nchi wanachama wa kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi zimeazimia kufuatilia juhudi za kutupilia mbali sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara na kiuchumi.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 19, 2024 04:44 UTC
  • Wanachama wa BRICS wameamua kufuta sarafu ya dola katika miamala ya kibiashara

Iran imesema nchi wanachama wa kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi zimeazimia kufuatilia juhudi za kutupilia mbali sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara na kiuchumi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani alisema hayo Jumamosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kando ya Kongamano la 15 la Kimataifa la Kiuchumi la " Russia na Ulimwengu wa Kiislamu: Jukwaa la Kazan 2024" huko Kazan, Jamhuri ya Tatarstan katika Shirikisho la Russia.

Amesema wanachama wa BRICS wamedhamiria kwa dhati kupunguza utegemezi wa dola ya Marekani lakini wanatakiwa kuandaa miundombinu muhimu katika nyanja mbalimbali ili kufanikisha jambo hilo.

Aliongeza kuwa wataalam wa mataifa ya BRICS wanafanya mashauriano ya mara kwa mara ili kuanzisha mifumo ya kufikia lengo la kuondoa dola katika kundi hilo.

BRICS awali ilijumuisha Brazil, Russia, India, China, Afrika Kusini na mwaka huu ilipanuka na kujumuisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu. BRICS sasa inawakilisha asilimia 45 ya watu duniani, asilimia 25 ya biashara ya kimataifa, asilimia 40 ya uzalishaji wa mafuta duniani na asilimia 28 ya Pato Ghafi la Taifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani (wa pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari mjini Kazan, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Mei 18, 2024 kando ya Kongamano la 15 la Kimataifa la Kiuchumi "Ulimwengu wa Kiislamu na Russia."

Muungano huo mpya umezidi kuwa muhimu katika kushughulikia maswala ya kimataifa tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2006, na mara nyingi unaonekana kuwa ulio dhidi ya satwa ya kiuchumi ya madola ya Magharibi.

Kwingineko katika matamshi yake, Bagheri Kani amesema ushirikiano kati ya Iran na Russia hauna madhara kwa nchi yoyote bali utakuza ustawi wa mataifa hayo mawili pamoja na amani na utulivu wa kieneo.

Akiashiria uwezo mkubwa wa Tehran na Moscow wa kuimarisha ushirikiano, mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa, pande hizo mbili zimeazimia kuvunja ukiritimba wa nchi za Magharibi katika masuala ya uchumi wa dunia na kuandaa mazingira ya kustawisha maingiliano kati ya madola huru.