Helikopta ya Rais Ebrahim Raisi haijulikani ilipo, timu za uokoaji zinaendelea kutafuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111948-helikopta_ya_rais_ebrahim_raisi_haijulikani_ilipo_timu_za_uokoaji_zinaendelea_kutafuta
Habari ambazo hazijathibitishwa zinaripoti kuwa helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanguka katika eneo la Jolfa, kaskazini magharibi mwa Iran.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 19, 2024 12:02 UTC
  • Raisi Ebrahim Raisi
    Raisi Ebrahim Raisi

Habari ambazo hazijathibitishwa zinaripoti kuwa helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanguka katika eneo la Jolfa, kaskazini magharibi mwa Iran.

Kulingana na shirika la habari la IRIB, maafisa wa serikali ya Iran wanasema, juhudi za timu za uokoaji za kutafuta eneo la ajali bado zinaendelea.

Hali mbaya ya hewa na ukungu mkubwa umefanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu katika eneo la Jolfa huko kaskazini maghaibi mwa Iran.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Ahmadi Vahidi amesema katika mahojiano na shirika la habari la IRIB kuwa timu za uokoaji bado hazijafika eneo la ajali na kuongeza kuwa, kumefanyika mawasiliano na baadhi ya watu waliokuwa katika msafara wa Rais, lakini hali mbaya ya hewa inatatiza juhudi za kufika eneo la ajali.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran amesema, msafara wa Rais Ebrahim Raisi ulikuwa angani katika helikopta kadhaa, na kwamba moja ya helikopta hizo ambayo ilimbeba Rais ililazimika kutua kwa kishindo kutokana na hali mbaya ya hewa.

Helikopta hiyo ilikuwa imembeba Raisi Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, Gavana wa mkoa wa Azarbaijan Mashariki Malek Rahmati, Imam wa Swala ya Ijumaa wa mji wa Tabriz Mohammad Ali Al- Hashem na maafisa wengine kadhaa.

Habari kamili kuhusu tukio hili itawajieni baadaye.