Eslami: Shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa mujibu wa sheria
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema: Shughuli za nyuklia za Iran zinafanayika ndani ya fremu ya sheria ya kimkakati ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislami (Bunge la Iran) kwa lengo la kuondoa vikwazo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB; Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebainisha kuwa ripoti za Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa Baraza la Magavana au Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zina sehemu mbili, kwanza ni kuhusu Mapatano ya Nyuklia ya JCPOA ya Iran na madola makubwa duniani na pili ni kuhusu hatua za kuhakikisha shughuli za nyuklia hazikengeuki mkondo. Kuhusu nukta hii amesema hatua zimechukuliwa kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia usambazwaji silaha za nyuklia NPT.
Aidha amekumbusha kuwa kwa kutilia maanani kuwa upande wa pili hususan Marekani haujatekeleza ahadi zake katika mapatano ya JCPOA, Jamhuri ya Kiislamu itatekeleza ahadi zake pale tu upande huo utakapoamua kutekeleza ahadi zake.

Kwa mujibu wa mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Tehran inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya JCPOA na haikubali shughuli yoyote ya nyuklia ambayo itadhuru mwingiliano kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza kwamba imeendeleza ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ndani ya fremu ya makubaliano yaliyopo na kwamba masuala yaliyosalia yanaweza kutatuliwa kwa njia ya kitaalamu iwapo IAEA itadumisha sera ya kutopendelea upande wowote.