Iran yamfahamisha Katibu Mkuu wa UN kuwa itawaadhibu 'Wazayuni wahalifu'
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani amesisitiza "haki ya asili" ya Iran ya kujilinda na kuchukua hatua za kujibu baada ya Israel kumuua Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palaestina, Hamas, mjini Tehran.
Bagheri Kani aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, jana Alhamisi, siku moja baada ya Haniyeh kuuawa katika kitendo cha kigaidi cha Israel. Ameongeza kuwa: "Kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni cha kumuua Ismail Haniyeh mjini Tehran si tu kwamba kimekiuka mamlaka ya kitaifa ya Jamhuri ya Kiislamu, bali pia kimehatarisha amani na usalama wa kieneo na kimataifa."
Amesisitiza kuwa: "Iran haitaacha haki yake ya asili ya kujilinda na kuchukua hatua za kujibu za kuwaadhibu Wazayuni wahalifu."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza pia ulazima wa kufanyika kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ili kulaani na kukabiliana na vitendo vya jinai vya utawala ghasibu wa Israel
Haniyeh, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, aliuawa pamoja na mlinzi wake, katika shambulio la Israel kwenye makazi yake kaskazini mwa Tehran mapema Jumatano.
Kitendo hicho cha kigaidi kilikuja saa chache baada ya Israel kumuua Fuad Shukr, kamanda mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon mjini Beirut.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa upande wake amelaani mashambulizi hayo mawili ya utawala wa Israel huko Beirut na Tehran.
Wakati huo huo, amekiri kwamba chini ya sheria za kimataifa, Iran ina haki ya kujilinda kihalali katika kukabiliana na ukiukwaji wa usalama wake wa taifa
Mwishoni mwa mazungumzo hayo, Bagheri Kani alisema jamii ya kimataifa inapaswa kuishinikiza Israel ikomeshe uhalifu wake huko Gaza, ambako vita vya mauaji ya halaiki ya Israel vimewauwa Wapalestina wasiopungua 39,480 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.