Iran: Serikali, mataifa na mashirika yote yawajibike kuhusu maafa ya Gaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa serikali na mataifa yote na mashirika ya kimataifa yanapaswa kuwajibika kuhusu maafa ya kutisha yanayoendelea hivi sasa katika Ukanda wa Gaza, na iwapo hayatachukua hatua, basi yatalaaniwa milele na kustahili kulaumiwa katika mahakama ya historia na dhamiri ya binadamu.
Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba: "Kutokana na utepetevu wa kushangaza wa mabaraza na jumuiya za kimataifa zinazowajibika na pia nchi za Kiarabu na Kiislamu kutochukuliwa hatua madhubuti, na chini ya moto wa uungaji mkono usio na kikomo wa silaha za Marekani na waitifaki wake wa kimagharibi kwa utawala kibaguzi wa Kizayuni, idadi ya mashahidi huko Gaza sasa imepindukia watu elfu arubaini."
Katika mauaji hayo ya kimbari ya Israeli dhidi ya Wapalestina wa Gaza, taakriban mashahidi 15,000 ni watoto, na miili ya mashahidi wapatao 10,000 wa Kipalestina pia imezikwa chini ya vifusi.
Kan'ani ameendelea kuhoji: "Ili kuziamsha dhamiri za wanadamu zilizolala duniani na kuwafanya viongozi na maafisa wa nchi na mashirika ya kimataifa wakose usingizi, je, takwimu hizi hazitishi na mnasubiri ziendelee kupanda?
Aidha mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran amesema ni kilele cha aibu kwa ulimwengu unaoonekana kustaarabika leo na kwa taasisi za kimataifa kwamba utawala bandia wa Israeli umekejeli kanuni na sheria zote za kimataifa mbele ya macho ya ulimwengu kwa kutekeleza mauaji ya kimbari bila kujali lolote dhidi ya taifa kongwe na kihistoria.
Tangu tarehe 7 Oktoba 2023 utawala wa kimbari wa Israel ukiungwa mkono kikamilifu na Marekani na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi ulianzisha mauaji makubwa katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina. Kimya cha jumuiya ya kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai za utawala ghasibu wa Israel ni chanzo cha kuendelea mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni.