Iran yasema magaidi wa MKO watashindwa kufikia malengo
Iran imelaani vikali uungaji mkono wa kisiasa na kifedha wa nchi za Magharibi kwa kundi la MKO, ikisema ndoto za kipuuzi na potofu za magaidi wa kundi hilo na wafuasi wao hazitatimia kamwe.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan’ani ametoa tamko hilo katika chapisho kwenye akaunti yake rasmi ya X siku ya Alhamisi kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Mapambano dhidi ya Ugaidi.
Siku hiyo huadhimishwa kama kumbukumbu ya mauaji ya mwaka 1981 ya rais wa wakati huo wa Iran Mohammad-Ali Rajaei na waziri mkuu wake Mohammad-Javad Bahonar. Viongozi hao wawili na wengine kadhaa walikuwa wamekutana katika ofisi ya Tehran ya Waziri Mkuu wa Iran katika mkutano wa Baraza Kuu la Ulinzi la Iran wakati mlipuko wa bomu ulipolipua jengo hilo na wote wawili wakauawa shahidi.
Kan’ani ameashiria rekodi mbaya ya vitendo vya jinai vya MKO dhidi ya watu wa Iran na kusema kama mamluki wa tawala za Marekani na Israel, magaidi hao wameunda na kuendeleza ugaidi wa kiserikali wa tawala hizo mbili ambapo wamehusika katika kuwaua wanasayansi wa nyuklia wa Iran.
Ameongeza kuwa, ni fedheha kuwa kundi la MKO ambalo linaungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za binadamu na misaada yao ya kisiasa na kifedha kwa magaidi hao kumepelekea kuuawa shahidi watu 17,000 nchini Iran.