Iran yaghariki katika maombolezo ya Siku ya Kufariki Dunia Mtume Muhammad SAW
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i115930-iran_yaghariki_katika_maombolezo_ya_siku_ya_kufariki_dunia_mtume_muhammad_saw
Wananchi Waislamu wa Iran jana usiku na leo Jumatatu mchana wameshiriki katika maombolezo ya kukumbuka siku alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW katika kona zote za nchi hususan Misikitini, katika Haram na maeneo mengine ya ibada.
(last modified 2024-09-02T07:34:08+00:00 )
Sep 02, 2024 07:34 UTC
  • Iran yaghariki katika maombolezo ya Siku ya Kufariki Dunia Mtume Muhammad SAW

Wananchi Waislamu wa Iran jana usiku na leo Jumatatu mchana wameshiriki katika maombolezo ya kukumbuka siku alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW katika kona zote za nchi hususan Misikitini, katika Haram na maeneo mengine ya ibada.

Leo Jumatatu tarehe Pili Septemba 2024 imesadifiana na mwezi 28 Mfunguo Tano Safar ambayo ni siku ya kukumbuka alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW na kuuawa shahidi mjukuu wake, Imam Hassan al Mujtaba AS. 

Mtume Muhammad SAW alibaathiwa na kupewa Utume akiwa na umri wa miaka 40 na alitekeleza kwa haki, kiukamilifu na kwa uaminifu mkubwa mno jukumu hilo kwa muda wa miaka 23 hadi alipotakiwa na Allah kuiacha hii dunia na kurejea kwa Mola wake Mtukufu miaka 1435 iliyopita.

Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Muhammad SAW alipata umashuhuri kwa jina la Muhammad Mwaminifu.

Kama tulivyotangulia kusema, akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SWT alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga.

Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasio na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Mtume Muhammad SAW.

Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad SAW alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba yeye kama yeye hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.