Ayatullah Khatami: Israel inazidi kujiangamiza
(last modified Fri, 06 Sep 2024 11:00:53 GMT )
Sep 06, 2024 11:00 UTC
  • Ayatullah Khatami: Israel inazidi kujiangamiza

Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amegusia nasaha 13 za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kwa Serikali ya 14 ya Iran na kusema kuwa, mafanikio ya serikali hiyo yako chini ya kivuli cha kutekeleza kivitendo nasaha hizo za Kiongozi Muadhamu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika khutba za Sala ya Ijumaa ya leo ya hapa Tehran na sehemu nyingine ya khutba zake amesema kuwa, jinai kubwa mno zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza ni dhihirisho la wazi la kukaribia kujiangamiza kikamilifu utawala huo dhalimu. 

Ameashiria jinsi Israel ilivyoua shahidi zaidi ya Wapalestina 40,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo wasio na hatia na kusema kuwa, nduli hao Wazayuni wanakabiliwa na siku mbaya sana katika siku za usoni. 

Amesisitiza kuwa, maandamano ya kila kona ya dunia na hata ndani ya utawala wa Kizayuni wenyewe dhidi ya nduli na watenda jinai hao ni ushahidi wa wazi kwamba Israel inajipeleka yenyewe kwenye maangamizi. 

Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran vilevile amesisitiza kuwa, Mwenyezi Mungu anasikia kilio cha watu wanaodhulumiwa na yuko katika mawindo dhidi ya madhalimu. Ameongeza kuwa, siku tulizo nazo mbele yetu hivi sasa zinatukumbusha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuangamia madhalimu na watenda jinai.

Ameongeza kuwa, sunna hiyo ya Mwenyezi Mungu ni ya milele. Hata katika mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala pia hali ilikuwa ni hivyo hivyo, Yazid hakubakia. Hata Bani Abbas waliofanya jinai nao pia hawakubakia. Lililo muhimu kwetu ni kuwa na yakini na sunna hiyo ya Mwenyezi Mungu.