Vita vya kisaikolojia vya kukaririwa vya Wamagharibi dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i116362-vita_vya_kisaikolojia_vya_kukaririwa_vya_wamagharibi_dhidi_ya_iran
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, amekiri baada ya wimbi la habari za uwongo dhidi ya Iran kuwa hana ushahidi wowote kuhusu kutumwa Russia makombora ya Iran.
(last modified 2024-09-14T08:09:08+00:00 )
Sep 14, 2024 08:09 UTC
  • Vita vya kisaikolojia vya kukaririwa vya Wamagharibi dhidi ya Iran

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, amekiri baada ya wimbi la habari za uwongo dhidi ya Iran kuwa hana ushahidi wowote kuhusu kutumwa Russia makombora ya Iran.

Wiki iliyopita maafisa na vyombo vya habari vya Marekani vilianzisha wimbi la habari dhidi ya Iran kwamba Iran imeitumia Russia makombora ya balistiki. Pande hizo zilitangaza kuwa wanao ushahidi unaothibitisha kuwa Iran imetuma Russia makombora ya balistiki. 

Uwezo wa makombora wa Iran 

Baada ya kuenea taarifa hii, Marekani na nchi tatu za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zilitangaza kuwa  zinaliwekea vikwazo Shirika la Ndege la Iran Air. Iran sawa na nchi nyingine duniani zimekuwa na zingali zinashirikiana pakubwa na Russia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijeshi baada ya Russia kuanzisha oparesheni za kijeshi huko Ukraine. 

Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Nato pia zimekuwa na zinaendelea kushirikiana kijeshi na Russia. Uturuki ambayo ni kati ya nchi wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) na inayowania kuwa mwanachama katika Umoja wa Ulaya ina ushirikiano mkubwa na Russia hata hivyo hakuna ukosoaji wowote unaofanywa na Marekani na Ulaya dhidi ya nchi hiyo. 

Marekani na Ulaya zinauhesabu ushirikiano wa Iran na Russia baada ya vita vya Ukraine kuwa ni dhambi isiyosameheka na kuutaja kuwa tishio kwa Ulaya. Kuhusiana na hili, awali ndege zisizo na rubani za Iran (droni) na sasa makombora ya balistiki yanayodaiwa kutumwa huko Russia, yote haya yametajwa kuwa tishio kwa Ulaya. 

Hii ni katika hali ambayo Iran imesema mara kadhaa kuwa haiungi mkono upande wowote katika vita vya Ukraine. Ni kuhusiana na suala hilo ndipo Iran ikabainisha kuwa haijaipatia Russia misaada ya kijeshi baada ya nchi hiyo kuanzisha mashambulizi huko Ukraine. Viongozi mbalimbali wa Iran akiwemo Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wamesisitiza kuhusu sera zisizoegemea upande wowote za Iran baada ya  wimbi jipya la habari dhidi ya Iran kuhusu kutumwa makombora ya balistiki nchini Russia. Araqchi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: 'Kwa mara nyingine tena Marekani na Ulaya zimechukua hatua kwa kuzingatia taarifa ghalati na bila ya mantiki; Iran haijatuma makombora ya balistiki huko Russia.'

Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Vita vya Ukraine ni fursa nyingine kwa ajili ya Wamagharibi kuzidisha siasa zao za uhasama dhidi ya Iran. Hii ni katika hali ambayo Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ametilia mkazo sera za kupunguza hali ya mivutano, kushirikiana na kuzungumza ili kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali kikanda na kimataifa. Marekani na washirika wake wa Ulaya wanatumia kila fursa inayojitokeza kuidhihirisha Iran kuwa tishio katika eneo na ulimwenguni kwa ujumla. 

Moja ya sababu za suala hilo ni kuongezeka wimbi la mashinikizo ya kimataifa khususuan fikra za waliowengi duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni unaotekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Jjinai hizo zisingeendelea kutekelezwa hadi leo bila ya uungaji mkono na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi kubwa za Ulaya kama Uingreza, Ujerumani na Ufaransa. Nchi hizo zimeigeuzia kibao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti ni tishio kwa nchi za Ulaya ili kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusu uhakika wa mambo na jinai zinazotekelezwa na Wazyuni kila uchao huko Gaza. Taarifa ya uwongo kwamba Iran imetuma Russia makombora ya balistiki imetolewa kwa msingi wa wa malengo haya tajwa. 

Serikali za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeelekeza hujuma zao kwa nguvu ya makombora ya Iran pamoja na miradi ya nyuklia ya nchi hii inayotekelezwa kwa malengo ya amani na uungaji mkono wa Iran kwa mhimili wa muqawama mkabala wa chokochoko za Wazayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kama kisingizio cha kutekeleza sera zao za kiuhasama za kuidhihirisha Iran kuwa tishio katika eneo na duniani. Iran inastawisha sekta yake ya makombora lengo lkiiwa ni kuzuia tishio lolote la hujuma ya uvamizi dhidi yake. Katika muongo wa 80 Iran iliathiriwa na moja ya vita vivilivyodumu kwa muda mrefu sana na kusababisha hasara na maafa makubwa kuwahi kushuhudiwa katika vita vya karne ya ishirini. Katika vita hivyo vya kulazimishwa, Marekani na akthari ya serikali za Ulaya zilimuunga mkono kwa pande zote Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq.