Mkuu wa IAEA atembelea maonyesho ya mafanikio ya nyuklia ya Iran
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi ametembelea mafanikio ya Iran katika sekta ya nyuklia, na kusema Jamhuri ya Kiislamu imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali za sayansi.
Iran imepata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali za sekta ya nyuklia, zikiwemo za radiopharmaceutical, isotopu pamoja na sekta ya kilimo na matibabu. Grossi ameyasema hayo Jumatano alipotembelea banda la Iran pembezoni mwa Kongamano la 68 la Kawaida la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika mji mkuu wa Austria Vienna.
Aidha ameeleza matumaini yake kuwa Iran itaendelea kupata mafanikio zaidi ya nyuklia.
Wakati huo huo, msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Behrouz Kamalvandi, amesema mkuu wa IAEA anatazamiwa kuzuru Tehran wakati fulani hivi karibuni, lakini akasema hakuna tarehe maalum ambayo imepangwa kwa ajili ya safari yake hiyo.
Kamalvandi ameelezea matumaini yake kuwa ziara ya Grossi itatoa matokeo chanya kwa Iran, kuhudumia maslahi yake ya kitaifa na kutatua masuala ya kiufundi kati ya Tehran na wakala wa nyuklia wa Umoja wa Mataifa.
Iran imeongeza kasi ya shughuli zake za amani za nyuklia tangu 2019, baada ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kuiondoa Washington kwenye makubaliano ya nyuklia ya 2015, ambayo yanajulikana kama Mpango Kamili wa Utekelezaji (JCPOA), yaliyofikiwa chini ya mtangulizi wake Barack Obama.
Tehran ilianza kupunguza ahadi zake chini ya JCPOA katika mfululizo wa hatua zilizotangazwa kabla na za wazi baada ya kushuhudia kushindwa kwa pande nyingine kudhamini maslahi yake chini ya makubaliano hayo.