Iran: Usalama na amani ya Lebanon ni muhimu sana kwetu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aemsema kuwa, ni jambo lililo wazi kabisa kwamba Jamhuri ya Kiislamu haiwezi kukaa kimya mbele ya vita vikubwa na vya pande zetu nchini Lebanon.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa BRICS kilichofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York Marekani na kuongeza kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi 12 iliyopita na kushindwa jamii ya kimataifa kukomesha jinai hizo huko Ghaza na Lebanon ni jambo la kutisha na kwamba kamwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kukaa na kuangalia kwa macho tu vita vya pande zote dhidi ya Lebanon.
Kikao hicho cha BRICS kimehudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 10 wanachama wa kundi hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia jinsi Tehran ilivyo mwanachama amilifu katika pande zote zinazohusu kundi la BRICS na kutilia mkazo udharura wa kutumiwa mfumo wa mabadilishano ya fedha za kigeni kwa njia ya dijitali, kuanzishwa majukwaa na programu za pamoja za mawasiliano kwa ajili ya mabadilishano ya fedha baina ya mabenki ya nchi wanachama wa BRICS na masuala yote ambayo yatapelekea kuachana ni mifumo ya kikoloni na kiukandamizaji ya madola ya kibeberu ya Magharibi.
Vilevile amesisitiza kuwa, BRICS ni kundi la nchi zenye nguvu na uwezo mkubwa wa kuathiri milingano na matukio duniani, hivyo kuna wajibu wa kutumiwa vizuri fursa hiyo kadiri inavyowezekana.