Jumuiya ya Shanghai yalaani shambulio la Israel dhidi ya Iran
(last modified Sun, 03 Nov 2024 02:33:38 GMT )
Nov 03, 2024 02:33 UTC
  • Jumuiya ya Shanghai yalaani shambulio la Israel dhidi ya Iran

Wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai wametoa taarifa na kulaani vikali hatua ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran.

Taarifa hiyo imetolewa katika kikao cha dharura cha jumuiya hiyo kilichoitishwa na Iran ambapo wawakilishi wake wamesema kuwa, wanalaani vikali hatua ya hivi karibuni ya utawala ghasibu wa Israel ya kukiuka mamlaka ya kujitawala Iran kwa kushambulia baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kiislamu.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai pia zimeeleza kusikitishwa kwake na ongezeko la mvutano katika eneo la Asia Magharibi ambao ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa na kutaka kuchukuliwa kwa hatua za kivitendo za kuleta utulivu katika eneo hilo.

Itakumbukwa kuwa, Jumamosi asubuhi ya tarehe 26 Oktoba utawala wa Kizayuni wa Israel ulishambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam, ambapo askari wanne wa Iran waliuawa shahidi. Pamoja na hayo mfumo jumuishi wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliweza kukabiliana kwa mafanikio na hatua hiyo ya kichokozi ya utawala huo bandia.