Takhte Ravanchi: Sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran zitafeli
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesisitiza kuwa jitihada zote za kuiwekea Tehran mashinikizo ya juu zaidi zitafeli.
Majid Takhte Ravanchi ameeleza haya katika mahojiano aliyofanya na gazeti la Financial Times la Uingereza. Ravanchi amesema kuwa, ni mapema kuzungumzia matokeo ya uhusiano wa baadaye baina ya Iran na Marekani katika utawala wa Donald Trump.
A,esema: Kuhusu mazungumzo, ni muhimu kuzingatia sera ya Marekani na kuamua jinsi ya kukabiliana nayo. Hivi sasa, suala kuu ni mbinu ambayo serikali mpya ya Marekani itakuwa nayo kuhusu Iran, suala la nyuklia na usalama wa eneo la Magharibi mwa Asia.
Takhte Ravanchi amesema kuwa Iran imeachawazi mlango wa mazungumzo na serikali ya Trump na kwamba iwapo Trump ataamiliana tena na Iran kwa mabavu na mashinikizo ya kiwango cha juu, atakabiliwa pia na upinzani wa kiwango cha juu zaidi. Kwa sababu Iran itaendelea kukwepa vikwazo, kuwa na washirika tofauti wa kibiashara na kuimarisha uhusiano wa kikanda ili kudumisha amani na utulivu.
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amedokeza kuwa utawala wa kwanza wa Trump ulidai kwamba utaiburuta Iran kwenye meza ya mazungumzo, lakini ulishindwa. Ameeleza matumaini yake kwamba Donald Trump hatarudia kosa hilo kwa sababu matokeo yake hayatabadilisha lolote.