Iran: Ni aibu kwamba ulimwengu ‘umeshindwa' kuzuia jinai za Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesikitishwa jamii ya kimataifa kushindwa kusimamisha jinai za utawala haramu wa Israel huku Marekani ikiuunga mkono utawala huo.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameyasema hayo mjini Cairo siku ya Jumatano, akihutubia Kikao cha 21 cha Baraza la Mawaziri wa Kundi la Nchi Nane Zinazoendelea za Kiislamu, linalojulikana kama D8..
Aragchi amesema: "Jamii ya kimataifa imeshindwa kwa aibu kukomesha vitendo vya uchokozi, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni." Amesema hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na usaidizi wa kisiasa, kijeshi, kijasusi na kifedha na utawala wa Marekani kwa Israel.
Waziri huyo wa mambo ya nje ameashiria takriban miezi 15 ya mashambulizi ya utawala haramu wa Isarel dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambapo Tel Aviv imekuwa ikiendesha vita vya mauaji ya kimbari mbali na mashambulizi yake dhidi Lebanon na Syria.
Vita hivyo hadi sasa vimpelekea Wapalestina wasiopungua 46,000 kupoteza maisha, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Takriban watu 4,000 pia waliuawa wakati wa mashambulizi makali ya Israel dhidi ya Lebanon ambayo yalianza muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa mashambulizi ya kikatili dhidi ya Gaza, na kudumu hadi mwezi uliopita, wakati usitishaji wa mapigano ulipoanza kutekelezwa. Tel Aviv imekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano mara nyingi na kusababisha athari mbaya kwa watu wa Lebanon.
Zaidi ya hayo, utawala huo umezidisha mashambulizi yake mabaya dhidi ya Syria, hasa yakilenga miundombinu yake ya kijeshi, baada ya nchi hiyo kuchukuliwa na wanamgambo wa Damascus wanaoungwa mkono na Magharibi na Israel.
Araghchi vile vile alibainisha kuwa mkutano huo wa D8 umekuja wakati ambapo ulimwengu wa Kiislamu ulikuwa bado unateseka kutokana na ukatili usio na kifani kutoka kwa utawala huo.
Wakati huo huo Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema "kadiri tutavyoweza kuboresha uhusiano wetu na nchi za Kiislamu ndivyo tutakavyoweza zaidi kuzima njama za maadui dhidi yetu".
Rais Pezeshkian aliyasema hayo jana Jumatatu kabla ya kuondoka Tehran kuelekea Cairo, Misri, kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 11 wa D8 ambao unafanyika leo Alhamisi.