Utawala wa Kizayuni umeshindwa na Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon
Khatibu wa Muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake ya kijeshi mbele ya Muqawama wa Kiislamu na Hizbullah huko kusini mwa Lebanon na ndio maana adui Mzayuni amelazimika kukubali usitishaji vita.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Hujjatul Islam Sayyid Mohammad Hassan Abu Torabifard amesema hayo katika khutba yake ya leo ya Sala ya Ijumaa hapa Tehran na kuongeza kuwa, "Mwenyezi Mungu ameweka mienge miwili inayong'arisha njia ya mwanadamu na kumuongoza kwenye uchamungu na ukamilifu wa kibinadamu. Mwenge wa kwanza ni ule unaotia nuru ndani ya nafsi ya mwanadamu nao ni akili.
Amma mwenge wa pili ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika sehemu nyingine ya khutba zake za Ijumaa ya leo, Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amegusia kadhia ya Syria na kusema: "Matukio ya Syria yamekuwa ni moja ya maudhui kuu zilizojadiliwa kwenye duru za kisiasa na vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni."
Ameongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni ambao umekumbwa na misukosuko mikali baada ya kushindwa kukabiliana na Kimbunga cha al Aqsa umelazimika kusalimu amri mbele ya irada madhubuti mno ya mhimili wa Muqawama, ambao msingi wake ni fikra, imani, ustahimilivu, subira na imani ya kina na isiyotetereka ya kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu bila ya kusahau uungaji mkono mkubwa wa Waislamu na watu wenye fikra za kibinadamu kote ulimwenguni.
Hujjatul Islam Abu Turabifard amesisitiza kuwa: "Inatosha kuangalia matukio ya eneo hili kuweza kuelewa kazi kubwa iliyofanywa na Muqawama wa Kiislamu huko Syria na Iraq na hii ni fursa nzuri ya kuwaenzi na kuwakumbuka kwa wema mashahidi wa Kambi ya Muqawama wakiwemo Luteni Jenerali Qassem Soleimani na shahidi Mhandisi Mahdi.