Maandamano ya Bahman 22 ya kuadhimisha ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu yaanza nchini kote
(last modified Mon, 10 Feb 2025 07:42:42 GMT )
Feb 10, 2025 07:42 UTC
  • Maandamano ya Bahman 22 ya kuadhimisha ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu yaanza nchini kote

Maandamano ya Bahman 22 ya kuadhimisha miaka 46 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yameanza kote nchini Iran ikiwa ni pamoja na katika Jiji kuu la Tehran.

Asubuhi ya leo, Jumatatu ya tarehe 22 Bahman, 1403 inayosaidifiana na Februari 10, 2025, maandamanao ya kuadhimisha mwaka wa 46 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yalianza kote nchini, pamoja na katika njia 12 za mjini Tehran kuelekea Mnara wa Azadi (Uhuru).
 
Kuanzia mapema leo asubuhi, wananchi wa Tehran wameonekana kwenye barabara zinazoelekea katika Mnara wa Azadi, eneo zinakofanyika sherehe za kumbukumbu ya ushindi wa Mapinduzi hayo.
 
Rais Masoud Pezeshkian anatazamiwa kuhutubia sherehe hizo katika uwanja huo wa Mnara wa Azadi.
 
Aidha, kauli mbiu kuu ya maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mwaka huu, ambayo yamesadifiana na kuzaliwa kwa Imamu Mahdi (a.s.), imetangazwa na Baraza la Uratibu wa Tablighi za Kiislamu kuwa ni "Kuhudhuria Hadi Kudhihiri."
 
Onyesho la usomaji kasida kwa pamoja la wanafunzi 1,357 ambao ni mwaka yalipofanyika Mapinduzi ya Kiislamu kwa mujibu wa kalenda ya hijria shamsia nalo pia limepangwa kuwa sehemu ya ratiba za maadhimisho hayo.
 
Sherehe za maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zinafanyika pia katika miji yote, vitongoji na vijiji nchini Iran, ambapo waandishi wa habari na wapiga picha wapatao  7,200 wanatazamiwa kuakisi tukio hilo kuu la kitaifa.
 
Katika maandamano ya leo, mbali na bendera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na picha za Mashahidi wa Vita vya Kujihami Kutakatifu, Walinzi wa Haram Tukufu na wa Muqawama, waandamanaji wanaonekana wamebeba pia bendera za Hizbullah ya Lebanon, Palestina, Harakati ya Al-Hashdu-Shaa'abi ya Iraq na Yemen.../