Iran yalaani vikali vitisho vya Trump vya mashambulizi ya kijeshi
Iran imelaani vikali vitisho vya hivi karibuni vya Rais wa Marekani, Donald Trump, vya kuishambulia nchi hii kijeshi ambapo imeviitaja kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa.
Balozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani ametoa matamshi hayo katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama siku ya Jumatatu.
Iravani amesema kuwa tangu alipoingia madarakani, Trump amekuwa akipuuza na kukiuka kanuni zote za kimataifa kwa kutoa vitisho dhidi ya mataifa huru kwa matumizi ya nguvu.
Jumamosi, Trump alisema kuwa Iran itashambuliwa kwa mabomu iwapo haitafikia makubaliano na Marekani.
Katika mahojiano na NBC News, Trump alisema: “Iwapo hawatafanya makubaliano, kutakuwa na mabomu." . Pia alitishia kuiadhibu Iran kwa kile alichokiita “ushuru wa pili.”
Iravani amesema: “Matamshi haya ya hovyo na ya kichokozi ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa, hasa Kifungu cha 2(4), ambacho kinakataza wazi vitisho au matumizi ya nguvu dhidi ya mipaka au mamlaka ya kisiasa ya taifa lolote.”
Iravani amelitaka Baraza la Usalama kulaani kwa njia ya wazi vitisho vya Trump kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Ameonya kuwa kushindwa kwa Baraza kuchukua hatua kunaweza kusababisha madhara makubwa si kwa eneo la Mashariki ya Kati pekee bali pia kwa amani na usalama wa kimataifa.
Iravani amesitiza kujitolea kwa Iran kwa ajili ya amani, utulivu, na usalama wa kikanda, akieleza kuwa Tehran haina nia ya kuanzisha mzozo au kuongeza mvutano.
Ameonya kuwa Iran itajibu haraka na kwa uthabiti kwa kitendo chochote cha uchokozi au shambulio lolote kutoka kwa Marekani au wakala wake, utawala wa Kizayuni wa Israel.
Iravani amebainisha kuwa Washington itawajibika kikamilifu kwa madhara yoyote yatakayotokana na kitendo cha uhasama.