Zaidi ya Wairani 30,000 wamewasili Saudi Arabia kwa ajili ya Hija
Zaidi ya Wairani 30,000 wamewasili nchini Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya Hija ya kila mwaka, huku idadi hiyo ikitazamiwa kuongezeka katika siku zijazo.
Tangu kuanza kwa safari za Hija kutoka Iran tarehe 5 Mei, jumla ya waumini 30,283 wameingia katika ufalme huo. Wote wamesafiri kwa njia ya ndege zilizotua katika miji ya Madina na Jeddah.
Mchakato wa kupeleka mahujaji ulioanza siku kumi na mbili zilizopita umehusisha jumla ya makundi 207 yaliyoandaliwa rasmi.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi, zaidi ya Wairani 85,000 wanatarajiwa kuwasili Makkah kufikia tarehe 31 Mei kwa ajili ya kuanza ibada za Hija.
Timu za matibabu kutoka Iran zinazofuatana na mahujaji zimeripoti jumla ya wagonjwa 7,348 waliotibiwa kwa huduma za nje katika vituo vya afya vinavyoendeshwa na Iran. Watu wawili walihitaji kulazwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Hakuna vifo vilivyoripotiwa miongoni mwa mahujaji wa Kiirani hadi sasa.
Katika siku za hivi karibuni, mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziyara za Kidini Iran alitembelea maeneo matakatifu ya Mina na Arafat kwa ajili ya kukagua maandalizi. Afisa huyo alikagua mifumo ya baridi na miundombinu ya usafi iliyowekwa kwa ajili ya mahujaji wa Iran katika kambi hizo.
Ibada ya Hija, ambayo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani, huwaleta pamoja mamilioni ya Waislamu kutoka kila kona ya dunia kila mwaka huko Makkah.