Bunge: Iran haitakubali kuachia haki yake ya nyuklia
Wabunge wa Iran wameendelea kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitasalimu amri juu ya haki yake ya nyuklia chini ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), hususan haki yake ya kurutubisha urani, huku wakikataa matakwa ya Marekani yaliyowasilishwa kupitia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, wabunge walijibu matamshi ya hivi karibuni yaliyotolewa na mwakilishi mkuu wa Marekani katika amzungumzo hayo, Steve Witkoff, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, ambao wamesisitiza kuwa Iran haipaswi kuwa na haki ya kurutubisha madini ya urani chini ya mpango wowote utakaochukua sehemu ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.
Taarifa hiyo imesema: “Tukiwa wajumbe katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), tunakataa kabisa madai haya yasiyo na msingi na ya kupotosha, na tunasisitiza kuwa utawala wa Marekani uko katika hatua ya kuporomoka, ukiwa dhaifu na usio na uthabiti."
Aidha taarifa hiyo imesema: “Utawala huu umejizatiti katika kuunga mkono ugaidi wa kitaifa na usio wa kitaifa. Ndani ya nchi yake, unakumbwa na maandamano ya wananchi katika majimbo kadhaa, huku kimataifa ukizozana na zaidi ya nchi 100 kutokana na sera zake za ushuru na hatua zake za upande mmoja.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa udhaifu wa utawala wa Marekani umeifanya ijiondoe kwa fedheha katika vita vilivyolazimishwa dhidi ya taifa la Yemen lenye ujasiri na uthabiti, ikirejelea kusitishwa kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Aidha, Bunge la Iran limesema kuwa licha ya vitisho vikali dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, na kuweka muda wa mwisho wa miezi kadhaa kwa ajili ya kuachiliwa mateka wa Kizayuni, Marekani hatimaye haikuwa na chaguo lingine ila kuingia katika mazungumzo na Hamas, na badala yake, kuruhusu kupitishwa kwa msaada wa kibinadamu ili kuwezesha kuachiliwa kwa mfungwa mwenye uraia pacha.
Wabunge wameonyesha kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, anahitaji mafanikio ili kuhakikisha ushindi wa chama chake cha Republican katika uchaguzi ujao wa Kongresi, baada ya kushindwa kumaliza vita vya Ukraine pamoja na migogoro mingine, na ndiyo maana anashiriki mazungumzo na Iran.
Kadhalika, taarifa hiyo imesisitiza kuwa shughuli za nyuklia na juhudi za urutubishaji wa urani za Iran ni halali, ziko ndani ya misingi ya kisheria, na zinazingatia kikamilifu masharti ya NPT na sheria za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Hatimaye, wabunge wameapa kuwa “matamshi matupu ya wahalifu hawa” hayawezi kuwa na athari yoyote kwa sera za Iran, na kwamba hawatakubali aina yoyote ya uingiliaji au tabia za kiburi kutoka kwa mahasimu wa taifa lao.