Iran yakanusha madai ya Trump kuhusu kutengeneza silaha za nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130010-iran_yakanusha_madai_ya_trump_kuhusu_kutengeneza_silaha_za_nyuklia
Iran imekanusha tuhuma zilizotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa taifa hili, ikisema madai hayo yametegemea kauli zilizopitwa na wakati ambazo zilitolewa na raia wa kawaida wa Iran.
(last modified 2025-08-26T09:09:40+00:00 )
Aug 26, 2025 06:04 UTC
  • Iran yakanusha madai ya Trump kuhusu kutengeneza silaha za nyuklia

Iran imekanusha tuhuma zilizotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa taifa hili, ikisema madai hayo yametegemea kauli zilizopitwa na wakati ambazo zilitolewa na raia wa kawaida wa Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, aliandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumatatu, akiashiria ujumbe wa hivi karibuni wa Trump katika vyombo vya habari ambapo aliishutumu Iran kwa kutaka kutengeneza silaha za nyuklia.

Baghaei amesema kuwa shutuma hizo ziliibuka kutokana na kauli zilizotolewa miaka iliyopita na raia wa Iran, ambazo tayari zimekanushwa mara kwa mara na maafisa wa ngazi za juu wa Iran na hata baadhi ya maafisa wa Marekani.

Amesisitiza kuwa madai ya Trump ni sehemu ya juhudi zake za kuhalalisha shambulio lisilo la kisheria la Marekani dhidi ya mitambo ya nyuklia ya amani ya Iran na pia kuunga mkono hatua za kijeshi za Israel dhidi ya taifa hili.

Aidha, ameashiria ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani, ambaye alithibitisha kuwa taasisi za kijasusi nchini humo bado zinakadiria kuwa Iran haijafanya juhudi za kutengeneza silaha za nyuklia.

Baghaei ameongeza kuwa, katika harakati za kuishutumu Iran, Trump anapuuzia ushahidi wa Mbunge wa Marekani Tulsi Gabbard uliotolewa mbele ya Bunge mnamo Machi 2025, na badala yake anategemea uchambuzi wa kibinafsi wa raia wa Iran kutoka mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Baghaei, mtazamo huo unaonesha wazi kuwa madai ya Trump yametegemea zaidi  misingi ya kisiasa kuliko uhalisia wa mambo.

Maafisa wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba taifa hili halina dhamira ya kutafuta silaha za nyuklia. Aidha Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ametoa Fatwa au hukumu ya kidini kuhusu uharamu wa kumiliki silaha za nyuklia.

Trump

Mnamo Juni, utawala wa Kizayuni wa Israel ulitekeleza mashambulizi ya kikatili ndani ya ardhi ya Iran, ukilenga makamanda wa kijeshi wa ngazi za juu, wanasayansi wa nyuklia pamoja na raia.

Vilevile, Israel ilishambulia kwa makusudi kituo cha nyuklia cha Natanz kilichopo katika mji wa Isfahan, kitendo kilicholaaniwa vikali duniani kwa kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria zote za kimataifa.

Kufuatia mashambulizi hayo, Iran ilianzisha operesheni ya kujibu mashambulizi kwa jina la ‘Ahadi ya Kweli III’ kama hatua ya kujilinda. Vikosi vya Ulinzi vya Iran vilivurumisha mamia ya makombora ya masafa marefu pamoja na ndege zisizo na rubani katika kukabiliana na mashambulizi ya kichokozi ya Israel. Marekani kisha iliingia vitani kwa maslahi ya Israel na kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Katika kujibu uchokozi huo vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilitekeleza pia operesheni ya shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha jeshi la anga cha Marekani cha Al-Udeid kilichoko nchini Qatar.

Hali hiyo ililazmisha utawala wa Kizayuni na Marekani  kuomba kusitishwa kwa mapigano baada ya siku 12 pekee.