Araqchi: Hatua ya Australia ya kumfukuza balozi wa Iran ni kutaka kuiridhisha Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani uamuzi wa Australia wa kumfukuza balozi wa Tehran nchini humo kutokana na madai eti ya mashambulizi kwenye vituo vya Kiyahudi, na kueleza kuwa ni kitendo cha kutaka kuiridhisha "serikali inayoongozwa na wahalifu wa kivita."
Katika ujumbe wake uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumanne, Abbas Araqchi alipinga madai ya Canberra, akiashiria ulinzi wa muda mrefu wa Iran kwa jamii ya Mayahudi hapa nchini.
"Iran ni nyumbani kwa moja ya jamii kongwe zaidi za Mayahudi duniani, ikiwa ni pamoja na makumi ya masinagogi. Kuishutumu Iran kuwa imeshambulia vituo kama hivyo nchini Australia, wakati sisi wenyewe tunafanya kila tuwezalo kuvilinda katika nchi yetu, hakuna maana yoyote," amesema Abbas Araqchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema "Iran inalipa gharama ya uungaji mkono wa watu wa Australia kwa Palestina", akimaanisha kuongezeka kwa maandamano ya kuitetea na kuiunga mkono Palestina kote nchini Australia kufuatia vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza.
Mapema jana Jumanne, Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese aliishutumu Iran kuwa ilipanga mashambulizi mawili kwenye maeneo ya Wayahudi mwezi Oktoba na Desemba, madai yaliyotolewa bila kuwasilisha ushahidi.
Ripoti za vyombo vya habari zinasema hatua hiyo imechukuliwa kwa ajili ya kukabiliana na ukosoaji wa Israel kwa serikali ya Albanese.
Mvutano kati ya Israel na Australia tayari umekuwa ukiongezeka baada ya Canberra kutangaza mapema mwezi huu kuwa itaungana na Ufaransa na mataifa mengine katika kulitambua rasmi taifa la Palestina kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi Septemba.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alijibu uamuzi huo, akimtuhumu Albanese kuwa "ameisaliti Israel", "kuwatelekeza Wayahudi wa Australia" na kwamba ni "mwanasiasa dhaifu."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema "hana na mazoea ya kujumuika na Wahalifu wa Kivita wanaosakwa (na mahakama za kimataifa), lakini Netanyahu yuko sahihi kuhusu jambo moja: Waziri Mkuu wa Australia ni 'mwanasiasa dhaifu'."