Waziri wa Ulinzi: Vikosi vya Iran vilipenya mifumo ya ulinzi wa makombora ya Israel
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesifu uwezo wa hali ya juu wa kijeshi wa taifa hili wakati wa vita vya siku 12 vya uchokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel, akisema kuwa Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viliweza kupenya mifumo ya ulinzi yenye tabaka nyingi ya utawala wa kichokozi wa Israel na kusambaratisha ngome kadhaa za kijeshi kwa kutumia makombora ya kisasa.
Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh alitoa kauli hiyo Jumanne alipokuwa akibainisha mafanikio ya sekta ya ulinzi ya Iran na namna nguvu za kijeshi za taifa hili ziliyodhihirika katika mashambulizi ya Marekani na Israel.
Waziri huyo wa Ulinzi wa Iran pia amesifu moyo wa kujitegemea wa vikosi vya Iran, pamoja na msisitizo wa kutumia maarifa, ubunifu wa kudumu, na teknolojia mpya, sambamba na miongozo ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika kuhakikisha vikosi vinaendelea kuwa tayari kukabiliana na tishio lolote la adui.
Mnamo Juni 13, Israel ilianzisha uvamizi wa wazi na wa kichokozi dhidi ya Iran, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 1,064, wakiwemo makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida.
Marekani nayo iliingia vitani kwa kushambulia maeneo matatu ya nyuklia ya Iran, kitendo kilichokiuka kwa kiwango kikubwa sheria za kimataifa.
Katika kujibu, Vikosi vya Jeshi la Iran vililenga maeneo ya kimkakati ndani ya ardhi inayokaliwa kwa mabavu pamoja na kambi ya kijeshi ya al-Udeid nchini Qatar, kambi kubwa zaidi ya Marekani katika eneo la Asia ya Magharibi.
Mnamo Juni 24, Iran, kupitia mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyoandaliwa kwa mafanikio dhidi ya utawala wa Israel na Marekani, iliweza kumlazimisha adui atangaze kusitisha uchokozi huo wa kigaidi.
Wakati huo huo, Kamanda wa Jeshi Meja Jenerali Amir Hatami amesema Jumatano kuwa Iran inapaswa kuwa na jeshi lenye nguvu ili kulilinda taifa, akiongeza kuwa nchi haina budi ila kujiimarisha zaidi katika mazingira ya sasa.