Araghchi: Iran na IAEA zinakaribia kuunda fremu mpya ya ushirikiano
Iran imesema imekaribia sana kubuni mfumo mpya wa ushirikiano baina yake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), miezi kadhaa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi hii kuipelekea Tehran kusimamisha ushirikiano wake na taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi aliyasema hayo katika hotuba yake kwenye kongamano la kitaifa kuhusu fursa za uwekezaji katika Maeneo Huru ya Iran mjini Tehran jana Jumamosi ambapo amesisitiza kuwa: Iran na IAEA zinakaribia kuunda fremu mpya ya ushirikiano
Ameeleza kuwa, mashambulizi ya Marekani kwenye vituo vyya nyuklia vya Iran mwezi Juni mwaka huu yalivuruga ushirikiano wa Tehran na IAEA na kuongeza kuwa, "Tunahitaji mfumo mpya wa ushirikiano na wakala huo. Kwa bahati nzuri, mazungumzo yetu na IAEA yameanza."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amebainisha kuwa, fremu mpya ya ushirikiano na IAEA itashughulikia masuala yote ya nchi, ikiwa ni pamoja na sheria ya Bunge iliyoidhinishwa kukabiliana na mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Kabla ya hapo, Araghchi alisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa liidhinishe juhudi za kidiplomasia katika kushughulikia mpango wa nyuklia wa Tehran na kukomesha vitendo vya "kinyume na sheria" vya Ulaya.
Araghchi ameyasema hayo katika mazungumzo tofauti aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki George Gerapetritis, wa Slovenia Tanja Fajon na wa Sierra Leone Alhaji Timothy Musa Kabba, ambao nchi zao ni wanachama wa zamu wa Baraza la Usalama.
Hali kadhalika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko imara katika kutetea haki zake za kisheria. Araghchi amesema Troika ya Ulaya - Ufaransa, Ujerumani na Uingereza - ilifanya "kosa kubwa" kwa kuamilisha kile kinachoitwa utaratibu wa 'snapback' kurejesha wa vikwazo dhidi ya Iran.