Je, ulinzi wa anga wa Yemen unaweza kuwa tishio kwa ndege za F-35 za Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i126516-je_ulinzi_wa_anga_wa_yemen_unaweza_kuwa_tishio_kwa_ndege_za_f_35_za_marekani
Marekani ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Yemen Machi 15, mwaka huu, ambayo ilikuwa operesheni muhimu zaidi ya kijeshi ya Marekani Asia Magharibi tangu Rais Donald Trump wa Marekani aingie tena madarakani.
(last modified 2025-05-18T02:28:47+00:00 )
May 18, 2025 02:28 UTC
  • Je, ulinzi wa anga wa Yemen unaweza kuwa tishio kwa ndege za F-35 za Marekani?

Marekani ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Yemen Machi 15, mwaka huu, ambayo ilikuwa operesheni muhimu zaidi ya kijeshi ya Marekani Asia Magharibi tangu Rais Donald Trump wa Marekani aingie tena madarakani.

Katika mashambulizi hayo, Jeshi la anga na la Wanamaji la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo mbalimbali ya Yemen zaidi ya mara elfu moja. Wamarekani walitumia ndege zilizoko kwenye manowari za Harry Truman na Carl Vinson kulenga maeneo mbalimbali ya Yemen zaidi ya mara elfu moja. Pamoja na hayo lakini Wamarekani walitambua mara moja kwamba walikuwa na kazi ngumu sana mbele yao ya kuharibu uwezo wa kijeshi wa Ansari Allah wa Yemen.

Kuendelea kushindwa pamoja na kuongezeka kwa hasara za kijeshi za Marekani na uwezekano wa kutunguliwa ndege za kivita za Marekani za kisasa, hasa ndege za kivita za F-35 za kizazi cha tano, kuliipelekea Ikulu ya White House, kubadilisha ghafla msimamo wake na kutangaza kwamba ilikuwa imeamua kusitisha mapigano katika vita vya Yemen ambapo Rais Trump wa Marekani alisimamisha operesheni zake za kijeshi nchini humo Mei 8. NBC iliripoti kuwa operesheni hiyo iliigharimu Marekani zaidi ya dola bilioni moja tangu mwezi Machi, ikiwa ni pamoja na maelfu ya mabomu na makombora yaliyotumika katika mashambulizi hayo. 

Gazeti la The New York Times, katika makala yenye kichwa cha habari "Kwa Nini Trump Aliamuru Ghafla Kusitishwa Mashambulio dhidi ya Wahouthi", lilitaja sababu za kusitishwa ghafla mashambulizi hayo kuwa zilitokana na matokeo yaliyotarajiwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja. Baada ya kutumia dola bilioni 1 na kupoteza idadi ya ndege za kivita aina ya F/A-18 Super Hornet, pamoja na idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani za MQ-9 Reaper, subira ya Trump ilifikia kikomo. Sehemu nyingine ya ripoti hiyo inasema kuwa Wayemeni walihatarisha maisha ya askari wa Marekai kwa kurusha makombora ya kutungulia ndege dhidi ya ndege za kivita za Marekani na hivyo kumpelekea Trump kuchukua uamuzi mgumu wa kusimamisha mashambulizi dhidi ya Wahouthi. Hili lilifanyika kwa upatanishi wa Oman, ambapo ilikubaliwa kwamba Wayemen hawatalenga meli za Marekani, nao Wamarekani hawataanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Wayemen. Mara kadhaa ndege za kivita za Marekani F-35 na F-16 zilikaribia kutunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Yemen, na kuathiri kwa kiasi kikubwa uamuzi wa Trump wa kusitisha kampeni ya kijeshi dhidi ya Yemen.

Wapiganaji wa Ansarullah

Swali ni je, ni mfumo gani wa kiulinzi na makombora gani yalitumiwa na Wayemen katika kukabiliana na ndege hizo hasimu za Marekani, ambayo yalizua hofu kubwa kwa Trump? Mwishoni mwa Agosti 2019, Wayemeni walizindua kombora lao la ulinzi, linalojulikana kama Fatir-1. Kombora hili linaonekana kuwa nakala mpya ya kombora la 3M9 la mfumo wa ulinzi wa anga wa SAM-6 uliotengenezwa na Umoja wa Soviet ya zamani na ulio na uwezo wa kulenga shabaha iliyo umbali wa takriban kilomita 25. Huu ni mfumo wa ulinzi wa masafa ya wastani ukiwa na rada uliotumika kuangusha ndege isiyo na rubani ya MQ-9 ya Marekani.

Wayemeni pia waliweza kutungua ndege kadhaa za Saudia, zikiwemo za F-15, Tornado na helikopta za mashambulizi za Apache, wakati wa vita na muungano wa kijeshi wa Saudia, wakiwa na ubunifu wao wa kubadilisha makombora ya masafa mafupi ya R-27 yaliyotengenezwa na Sovieti, kuwa makombora ya kutoka ardhini kuelekea angani.
Kuhusu  ndege ya F-35, ambayo ni ndege isiyoonekana kwenye rada, ndege hii kwa hakika ina uwezo mkubwa wa kukwepa na kutoonekana kwenye rada za aina nyingi. Pamoja na hayo, afisa mmoja wa Marekani alikiri katika mahojiano na tovuti ya "War Zone" kwamba ndege hiyo ililazimika kutumia mbinu nyingi za ziada ili kukwepa kutunguliwa na makombora ya ardhini kwa anga ya Yemen. Alisema: "Makombora yalikaribia sana hivi kwamba F-35 ililazimika kutumia mbinu za ziada kuyakwepa." Maafisa kadhaa wa Marekani pia walisema: "Ndege kadhaa za Marekani aina ya F-16 na F-35 zilikuwa karibu kulengwa na ulinzi wa anga wa muqawama wa Yemen, jambo ambalo lilifanya uwezekano wa kudhuriwa askari wa Marekani kuwa wa kweli kabisa."

Ubunifu wa Wayemen katika kutumia silaha walizonazo unapaswa kuzingatiwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyopelekea Washington kutathmini upya operesheni zake za kijeshi nchini Yemen na hatimaye kuzisimamisha. Kwa hakika Marekani ilipuuza kipengele muhimu katika operesheni za kijeshi nchini Yemen, yaani, weledi wa kijeshi wa jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansar Allah na kunufaika kwao na tajriba za vita vya muda mrefu vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen. Vyombo vya habari vya Magharibi, vilizua dhana potofu kwamba Wamarekani walikuwa wanakabiliana na watu wa enzi za jiwe wasio na ujuzi wala muundo wa kitaalamu wa kijeshi.

Wakati matokeo ya operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Yemen, ikiwa ni pamoja na kutunguliwa ndege zisizo na rubani 27 aina ya MQ-9 Reaper na muqawama wa Yemen na kugharamika Washington zaidi ya dola milioni 800 pamoja na ndege zake za kivita aina ya Marekani F-35 yalipodhihirika zaidi,  hapo ndipo viongozi wa Marekani walipoamka kutoka usingizini  na kutambua kwamba wapiganaji wa Yemen walikuwa na ujasiri na ushujaa mkubwa usioelezeka, pamoja na zana za kijeshi ambazo ziliwawezesha kutoa kipigo kikali dhidi ya Marekani na hatimaye kuilazimisha kukubali kusitisha vita dhidi ya taifa la Yemen.