Mkutano wa OIC mjini Jeddah wahimiza hatua ya pamoja kumaliza mauaji ya kimbari Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130008-mkutano_wa_oic_mjini_jeddah_wahimiza_hatua_ya_pamoja_kumaliza_mauaji_ya_kimbari_gaza
Mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano la Kiislamu (OIC) ulianza Jumatatu mjini Jeddah, Saudi Arabia, ambapo washiriki wamesisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua ya pamoja kwa ajili ya kusaidia Gaza na Palestina.
(last modified 2025-08-26T09:11:17+00:00 )
Aug 26, 2025 06:02 UTC
  • Mkutano wa OIC mjini Jeddah wahimiza hatua ya pamoja kumaliza mauaji ya kimbari Gaza

Mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano la Kiislamu (OIC) ulianza Jumatatu mjini Jeddah, Saudi Arabia, ambapo washiriki wamesisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua ya pamoja kwa ajili ya kusaidia Gaza na Palestina.

Lengo la mkutano huu ni kuchunguza njia za kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema katika hotuba yake kwamba kinachohitajika na watu wa Palestina ni hatua ya pamoja.

Fidan ameongeza kuwa utawala wa Israel unapaswa kushinikizwa kwa nguvu na kwa ushirikiano ili kupata suluhisho la kudumu la suala la Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan, pia amezungumza katika mkutano huo Jumatatu na kusema kwamba utawala wa Kizayuni unaleta tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.

Amesisitiza kuwa jamii ya kimataifa lazima imalize uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni na kuupinga.

Waziri bin Farhan ameisisitiza haki ya Wapalestina ya kuanzisha taifa lao huru.  Aidha ameunga mkono juhudi za Misri na Qatar za kufikia mapatano ya kusitisha mapigano Gaza, huku akilaani matamshi ya waziri mkuu wa Israel kuhusu mpango wa "Israeli Kubwa."

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, pia amezungumza katika mkutano huo na amesisitiza kwamba matamshi ya viongozi wa Israeli kuhusu kuanzisha "Israeli Kubwa" kutoka Mto Nile hadi Mto Euphrates yanalaaniwa kabisa, na kusema kuwa nchi za Kiislamu lazima zishirikiane zote kutokomeza itikadi ya kujitania Israel.

Mansour aliongeza kwamba kushindwa kwa jamii ya kimataifa kuwawajibisha viongozi wa Israeli kumewafanya kumewafanya wapate kiburi zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pia alizungumza katika mkutano wa OIC. Amelaani mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza na kusisitiza haja ya hatua za kukabiliana na utawala wa Kizayuni.  Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa kukomesha mauaji ya halaiki ya Israel yanayoendelea huko Gaza, akisema kuwa nchi zote zinapaswa kusimama upande sahihi wa historia ambao "hautasamehe" ucheleweshaji wowote zaidi wa kupunguza mateso ya watu wa Palestina.

Mkutano wa Dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC umefanyika kufuatia ombi la Iran, ambalo lilitumwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi kwa Katibu Mkuu wa OIC, mnamo tarehe 6 Agosti.