Uchunguzi wa maoni: Wanajeshi wengi wa Israel wanapinga kuendelezwa mashambulizi dhidi ya Gaza
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uuliyochapishwa Jumatatu wiki hii na Taasisi ya Utafiti ya Agam, Wazayuni walio wengi wanakubaliana kwa kauli moja katika suala la kuhitimishwa vita vya Gaza na kufikia makubaliano ya kina na harakati ya Hamas.
Chombo cha habari cha usalama cha Israel "Walla News" kimechapisha matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya utafiti ya Kizayuni ya "Agam" kuhusiana na kiwango cha uungaji mkono wa Waisraeli wa kusimamisha vita, yakionyesha kwamba wengi wao wanataka kuhitimishwa vita huko Gaza na kufikiwa makubaliano na harakati ya Hamas.
Walla news imeripoti kuwa: Kwa mujibu wa uchunguzi huo, asilimia 73.9 ya wanajeshi wa kawaida na wa akiba wa Israel wanataka vita huko Gaza vikome, na ni 26.1 pekee wanaoamini kuwa vita vya Gaza vinapaswa kuendelea hata kwa gharama ya kuhatarisha maisha ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa na wapigania ukombozi wa Palestina.
Zaidi ya hayo ni kwamba, asilimia 64 ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wanaamini kuwa vita vya Gaza vilianzishwa na vinaendelea kwa kuzingatia malengo ya kisiasa.
Walla imeripoti, ikinukuu uchunguzi wa Taasisi ya Agam, kwamba asilimia 40 ya wanajeshi wamepoteza motisha ya kupigana huko Gaza.
Haya yanajiri katika hali ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel unajiandaa kuukalia kwa mabavu Mji wa Gaza, na jeshi limewaita makumi ya maelfu ya askari wa akiba ili kupanua vita huko Gaza.