Hamas: Israel imechuja orodha ya Wapalestina wanaopasa kuachiwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i131820-hamas_israel_imechuja_orodha_ya_wapalestina_wanaopasa_kuachiwa
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema utawala wa Israel unajaribu kuhadaa, kufanyia hila na kuchuja baadhi ya vipengele katika makubaliano ya usitishaji vita.
(last modified 2025-10-10T09:12:57+00:00 )
Oct 10, 2025 06:55 UTC
  • Hamas: Israel imechuja orodha ya Wapalestina wanaopasa kuachiwa

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema utawala wa Israel unajaribu kuhadaa, kufanyia hila na kuchuja baadhi ya vipengele katika makubaliano ya usitishaji vita.

Kufuatia kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita huko nchini Misri hapo jana, Hazem Qasim amesema kuwa utawala wa Israel unajaribu kutumia vibaya vipengele vinavyohusiana na orodha ya wafungwa na kuondoka Gaza, na unakwepa mjadala kuhusu masuala hayo.

Qasim amesisitiza kuwa, suala la msingi ni kuandaa mazingira kwa ajili ya kubadilishana wafungwa na mateka. Ameeleza bayana kuwa, makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanamaanisha kumalizika kwa vita vya kikatili dhidi ya wananchi wa Palestina.

Chanzo kilicho karibu na mfungwa wa Kipalestina, Marwan Barghouti kimefichua kuwa ofisi ya waziri mkuu wa Israel iliondoa jina lake kwenye orodha ya kubadilishana wafungwa dakika za mwisho, na hivyo kuhujumu makubaliano hayo ya kusitisha mapigano Gaza.

Barghouti, mwanasiasa mashuhuri wa Palestina, alionekana kama shakhsia muhimu wa kuachia huru mkabala wa mateka 48 wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza, chanzo cha habari kimeiambia Middle East Eye. Barghouti anatazamwa kama mtu anayeunganisha sana jamii ya Wapalestina.

Hamas imetaka kuachiliwa kwa kiongozi huyo wa kundi la Fat'h aliyefungwa kwa muda mrefu pamoja na mateka wengine mashuhuri akiwemo Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PFLP) Ahmad Saadat, na mhandisi na kiongozi mkuu wa Brigedi za Qassam, Abdullah Barghouti. Kiongozi mwandamizi wa Hamas, Abbas al-Sayed pia yuko kwenye orodha hiyo.

Haya yanajiri huku baadhi ya ripoti zikieleza kuwa, jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi yake huko Gaza saa chache tangu Tel Aviv iidhinishe awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano na Hamas.

Kanali ya Al Jazeera ya lugha ya Kiarabu imeripoti kuwa, muda mfupi uliopita wanajeshi wa Israel wametekeleza wimbi la mashambulizi ya makombora na mizinga mikubwa ya vifaru kaskazini mwa mji wa Khan Younis, kusini mwa Gaza.