Israel yalaaniwa vikali kwa kuvamia ofisi za UNRWA Quds Mashariki
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, limesema kwamba polisi wa Israel walivamia makao yake makuu katika Quds (Jerusalem) Mashariki mapema Jumatatu, hatua ambayo limeitaja kuwa “changamoto mpya kwa sheria za kimataifa.”
Kwa mujibu wa Philippe Lazzarini, Kamishina Mkuu wa UNRWA, “maafisa wa usalama wa Israel, wakiwa wameambatana na maafisa wa manispaa, waliingia kwa nguvu kwenye majengo ya UNRWA, ambako walikata mawasiliano yote, kuchukua vifaa vya kompyuta, na kubadilisha bendera ya bluu ya Umoja wa Mataifa kwa bendera ya Israel.”
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Lazzarini amelaani vikali kitendo hicho akisema “Kitendo hiki kipya kinaonesha dharau ya wazi ya Israel kwa majengo ya Umoja wa Mataifa”.
Amesema Israel imekiuka wajibu wake wa kulinda ofisi za Umoja wa Mataifa.
Kabla ya hatua hii ya utawala wa Isarel, UNRWA imeshuhudia kuongezeka kwa shinikizo baada ya “miezi ya unyanyasaji na kampeni ya upotoshaji dhidi ya shirika hilo na vitisho vya mara kwa mara.”
Muhimu zaidi, amesema UNRWA inalengwa na sheria mbili zilizopitishwa na bunge la Israel, 'Knesset' mwezi Oktoba. Sheria ya kwanza inapiga marufuku shughuli za shirika hilo kote Israel, ikiwemo Quds Mashariki, na nyingine inamzuia afisa yeyote wa Israel kushirikiana na wafanyakazi wa UNRWA.
Chini ya shinikizo hili linaloongezeka, shirika lililazimika mwishoni mwa Januari kuhamisha makao yake makuu katika kitongoji cha Sheikh Jarrah na kupeleka kwa muda wafanyakazi wake wa kimataifa nchini Jordan.
Lakini Lazzarini amesisitiza kuwa “hakuna sheria ya kitaifa inayoweza kufuta hadhi ya kimataifa ya makao makuu ya UNRWA. UNRWA inabakia kuwa kituo cha Umoja wa Mataifa, na hivyo inalindwa dhidi ya aina yoyote ya kuingiliwa,”
Mahakama ya Kimataifa ya Haki yenyewe imesisitiza kuwa Israel ina wajibu wa kushirikiana na UNRWA.
Uvamizi huo wa Jumatatu unakuja siku tatu tu baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhuisha mamlaka ya UNRWA kwa miaka mingine mitatu. Uamuzi huo ulifikiwa kupitia kura ya wengi kwa kishindo, jambo ambalo Lazzarini amelisifu kama ishara ya mshikamano wa kimataifa usiotetereka.
Shule za UNRWA, pamoja kliniki na huduma za kijamii zinazotolewa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa, ambazo ni muhimu kwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina Mashariki ya Kati, zimekuwa kitovu cha mvutano ambapo sheria za kimataifa zinakutana uso kwa uso na ukaliaji mabavu wa Israel katika ardhi ya Palestina.