Mansur Hadi akiri Imarati imevamia maeneo ya kistratijia ya Yemen
Katika malumbano yake na Mohammed bin Zayed Al Nahyan, mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi na Naibu Kamanda wa Jeshi la Imarati, Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyetangaza kujiuzulu na kutoroka nchi amekiri kwamba nchi hiyo imeivamia kijeshi Yemen.
Mansur Hadi amesema kuwa, Imarati kupitia fremu ya upatanishi, inajishughulisha pia na kazi za kivamia nchini Yemen. Baada ya Saudi Arabia, Imarati ni nchi ya pili inayoshiriki pakubwa katika vita dhidi ya taifa la Yemen. Hata hivyo sambamba na malengo ya kisiasa nchini Yemen, pia inafuatilia malengo mengine ikiwa ni pamoja na kutwaa ardhi za nchi hiyo. Malengo makubwa ya kisiasa yanayofuatiliwa na Imarati nchini Yemen ni kuizuia harakati ya wananchi ya Answarullah kuwa na nguvu na ushawishi zaidi katika muundo wa serikali ya nchi. Hii ni katika hali ambayo Imarati inafanya njama ya kuzikalia kwa mabavu baadhi ya sehemu za Yemen na kuimarisha nafasi yake ndani ya taifa hilo la Kiarabu.
Ili kufanikisha malengo hayo, Imarati imepiga kambi katika maeneo ya kusini ya Yemen. Katika uwanja huo, sambamba na kufanya njama za kujidhihirisha kwa sura nzuri kati ya watu wa makabila ya maeneo ya kusini mwa Yemen, inayakalia pia maeneo ya kistratijia yenye utajiri wa mafuta. Aidha sambamba na kuwa na karibu askari 1500 nchini Yemen, pia imeajiri wapiganaji wa ndani ya nchi hiyo. Kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha, Abu Dhabi imeweza kuajiri wapiganaji wengi wa makabila ya kusini mwa Yemen ambapo huwapatia mafunzo ya kijeshi na kuwatumia wanamgambo hao kwa ajili ya kufikia malengo yake. Kwa mfano tu, Imarati kwa kutumia wapiganaji 3000 ilivamia miji miwili ya Azzan na Habban ya eneo la Shabwah, kusini mashariki mwa Yemen na kuikalia kwa mabavu, hatua ambayo ilienda sambamba na kudhibiti maene yenye utajiri wa mafuta na gesi ya eneo hilo.
Kama hiyo haitoshi Imarati pia imevikalia kwa mabavu visiwa vya Socotra, Darsah, Samha na Abdul Kuri na visiwa viwili vya miamba vilivyopo katika Bahari ya Hindi na karibu na Ghuba ya Aden. Ili kurahisisha uvamizi wake huo, Imarati imekuwa ikitoa uraia kwa wakazi wa visiwa hivyo na kuwanunua viongozi wa makabila yake.
Katika hali hiyo, sambamba na Abdrabbuh Mansur Hadi kutoridhishwa na mwenendo wa udhibiti wa serikali ya Abu Dhabi wa maeneo yenye utajiri wa mafuta, maeneo muhimu na ya kistratijia sambamba na kuzibadili baadhi ya kambi za kijeshi na kuzifanya kuwa jela zake za siri, amepinga pia hatua ya Imarati ya kutaka kuudhibiti uwanja wa ndege wa mji wa Aden. Ukweli ni kwamba, Abdrabbuh Mansur Hadi si kwamba amechukizwa na hatua ya Imarati kudhibiti baadhi ya ardhi za Yemen, bali kile kilichomtia hasira rais huyo wa zamani wa Yemen aliyetangaza kujiuzulu na kutoroka nchi ni kwamba, uwepo wa nchi hiyo huko Aden ni kinyume na maslahi yake binafsi ambapo hata kudhibitiwa uwanja wa ndege wa mji huo kumetatiza harakati zake.
Katika uwanja huo, vyombo vya habari vya upande wa Abdrabbuh Mansur Hadi mwezi Fubruari mwaka huu vilitangaza kuwa Imarati imezuia kutua ndege iliyokuwa imembeba rais huyo wa zamani wa Yemen na kibaraka wa Saudia katika uwanja wa Aden na kwamba Abu Dhabi inaongoza operesheni za uasi za makamanda waliomuasi Mansur Hadi.
Katika miezi iliyopita, Imarati sambamba na kuunda muungano wa kisiasa ulioitwa 'Azimio la Kihistoria la Aden' na kumteua Aidarus al-Zoubaidi, mkuu wa mkoa wa zamani wa Aden kama kiongozi wa muungano huo, pia imekuwa na tofauti kubwa na Mansur Hadi hasa baada ya rais huyo wa zamani wa Yemen kumpiga kalamu nyekundu Aidarus al-Zoubaidi.