Dec 02, 2025 02:39 UTC
  • Jumanne, tarehe Pili Disemba, 2025

Leo ni Jumanne tarehe 11 Jumadithani 1447 Hijria sawa na tarehe Pili Disemba 2025.

Siku kama ya leo miaka 1049 iliyopita aliaga dunia mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga wa Kiirani, Badiu Zaman al Hamadani.

Alizaliwa huko Hamedan magharibi mwa Iran na kupata umashuhuri kwa jila la Fadhil Hamadani. Badiu Zaman alibobea sana katika kuandika mashairi na nathari kwa lugha ya Kiarabu na alikuwa hodari mno katika utungaji wa mashairi.

Miongoni mwa vitabu vya malenga huyo wa Kiirani ni Rasaailu Dadiu Zaman. 

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza.

Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka.   

Mirza Kuchak Khan Jangali

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, Peninsula ya Korea iligawanywa katika sehemu mbili za kaskazini na kusini.

Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa Japan ambayo ilikuwa imedhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki mwa Asia, viongozi waitifaki walifanya vikao katika miji ya Yalta na Potsdam wakijadili juu ya namna ya kuongoza dunia baada ya kumalizika kwa vita hivyo.

Hata hivyo katika vikao hivyo kulibainika mapema kwamba Marekani na Urusi ya Mazani, zilikuwa zikiwania fungu kubwa zaidi kwa ajili ya kupenyeza siasa zao na kulidhibiti eneo tajwa. Hivyo eneo hilo na kwa mujibu wa mapendekezo ya viongozi wa nchi zilizoibuka washindi katika vita, likagawanywa sehemu mbili katika siku kama ya leo. 

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Laos ilipata uhuru kamili.

Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893.

Mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiwango fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China. 

Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba.

Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela.

Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni. Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya.

Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kutoroka nchi hiyo. 

Fidel Castro

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa.

Ni vyema kutaja hapa kuwa, tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia.

Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi.  ***

Na tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani.

Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo.