Ijumaa, Julai 31, 2026
Leo ni Iijumaa tarehe 16 Mfunguo Tano Safar 1447 Hijria, sawa na 31 Julai 2026.
Tarehe 31 Julai miaka 220 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza.
Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi.
Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa. *****
Katika siku kama hi ya leo miaka 140 iliyopita aliaga dunia Franz Liszt mtunzi wa nyimbo wa Hungary.
Franz alizaliwa mwaka 1811. Franz Liszt pia alikuwa na kipawa na maarifa makubwa katika utungaji wa nyimbo. Nyimbo Hungarian Rhapsodies na shairi la Symphony ni miongoni mwa kazi za utunzi wa Franz Liszt. ****
Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 9 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi mjini Tehran Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qajar nchini Iran.
Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba na alisimama kidete kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na miongozo na mafundisho ya Uislamu.***
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka.
Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta.
Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hazijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight." ****
Tarehe 31 Julai miaka 66 iliyopita kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad, alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo.
Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi.
Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad. ***
Miaka 46 iliyopita, tarehe 9 Mordad, 1359 Hijria Shamsia alama za bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambazo zilikuwa zimepasishwa hapo awali, zilitangazwa rasmi.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini (RA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, alitoa wito wa kubuniwa bendera ambayo ingeendana na maudhui na malengo ya Mapinduzi na utawala wa Kiislamu. Bendera iliyopitishwa, kama ilivyokuwa hapo awali, ina rangi tatu: kijani upande wa juu, nyeupe katikati, na nyekundu upande wa chini. Kijani ni rangi ya bendera ya Kiislamu na pia ishara ya kijani kibichi na ustawi wa Iran. Rangi nyeupe inawakilisha asili ya kupenda amani na usalama ya Wairani, na rangi nyekundu inaashiria damu na moyo wa kujisabilia kwao katika kutetea dini na nchi yao.
Katikati ya bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuna alama ya "Allah", ambayo ukiitazama kwa umakini zaidi inaweza kusomwa kama "La ilaha illallah".
Kifungu cha maneno: "Allahu Akbar" kimeandikwa mara 22 kandokando ya rangi mweupe ya bendera ya Iran, kikiashiria ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 22 mwezi Bahman 1357 Hijria Shamsia.
Kwa ujumla, bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawakilisha mafundisho ya Kiislamu yanayotawala Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. ***
Tarehe 9 Mordad mwaka 1366 Hijria Shamsia yaani siku kama ya leo miaka 39 iliyopita kulitokea tukio la kusikitisha la Ijumaa ya Damu mjini Makka.
Siku hiyo mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina ndani ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel.
Siku hiyo askari wa Kiwahabi wa Saudia walishambulia mahujaji hao kwa risasi na kuua mahujaji 400 za Kiirani na kujeruhi wengine zaidi ya elfu moja. *****