Ripoti ya polisi Kenya yafichua ukatili wa wanajeshi wa Uingereza Laikipia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140338-ripoti_ya_polisi_kenya_yafichua_ukatili_wa_wanajeshi_wa_uingereza_laikipia
Ripoti ya siri ya polisi ya Kenya imefichua madai mazito ya ubakaji, ulawiti wa watoto na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa kikosi cha Uingereza wanaopata mafunzo Kenya (BATUK) katika Kaunti ya Laikipia.
(last modified 2026-08-01T11:56:21+00:00 )
Aug 01, 2026 11:45 UTC
  • Wanajeshi wa Uingerea nchini Kenya
    Wanajeshi wa Uingerea nchini Kenya

Ripoti ya siri ya polisi ya Kenya imefichua madai mazito ya ubakaji, ulawiti wa watoto na ukiukaji wa haki za kibinadamu unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa kikosi cha Uingereza wanaopata mafunzo Kenya (BATUK) katika Kaunti ya Laikipia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Mei 19, 2026, iliyotiwa saini na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na kuwasilishwa bungeni, baadhi ya wanajeshi wa Uingereza walivuka kutoka eneo lao la mazoezi ya kijeshi hadi vijiji jirani na kuwashambulia raia.

Katika kijiji cha Lekiji, Kaunti Ndogo ya Laikipia Kaskazini, msichana mwenye umri wa miaka 12 anaripotiwa kubakwa mara kadhaa na wanajeshi hao baada ya kushawishiwa kwa peremendepipi alipokuwa akivua samaki karibu na mto.

Ripoti hiyo inadai kuwa baadaye msichana huyo alipata ujauzito na kujifungua mtoto mwenye asili mchanganyiko.

Watoto wengine, kwa mujibu wa uchunguzi huo, walinaswa kwa kupewa biskuti, chokoleti na vinywaji kabla ya kudhulumiwa kingono.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa manusura wengi walitelekezwa wakiwa wamepoteza fahamu na kuokolewa baadaye na jamaa, majirani au wachungaji wa mifugo waliosikia vilio vyao.

Katika Kaunti ya Laikipia pekee, polisi wa Kenya walirekodi visa vya watu 37 waliodaiwa kubakwa na genge la wanajeshi wa Uingereza, watu 20 kubakwa na wengine wawili kujeruhiwa walipokuwa wakijaribu kutoroka mashambulizi hayo.

Waathiriwa wameeleza kuwa washambuliaji walikuwa wamevalia sare za kijeshi na mara nyingi waliwashambulia katika maeneo yaliyotengwa kama vichakani, njia za porini na kandokando ya mito walipokuwa wakichota maji, kukusanya kuni, kuogelea au kuchunga mifugo.

Baadhi ya wanawake wamedai kuwa walipoteza mimba baada ya mashambulizi hayo huku wengine wakisema hawakuweza tena kupata ujauzito.

Wachunguzi wa polisi ya Kenya walichukua taarifa kutoka kwa manusura 40 wenye umri kati ya miaka 48 na 90 waliotoa ushahidi kuhusu ukatili huo pamoja na madhara ya muda mrefu ya kimwili na kisaikolojia.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa watoto waliozaliwa kutokana na visa hivyo wanakabiliwa na ubaguzi, unyanyapaa na kukosa msaada kutoka kwa wanaodaiwa kuwa baba zao. Polisi walitambua mtoto mmoja mwenye asili mchanganyiko Laikipia, huku ikielezwa kuwa sampuli za DNA za baadhi ya waathiriwa zilipelekwa Uingereza kwa uchunguzi kubaini baba mzazi.

Kutokana na matokeo hayo, polisi wanapendekeza serikali ichukue hatua za kisheria kupitia mikataba ya kimataifa ya usaidizi wa kisheria na pia kuendelea na uchunguzi wa DNA kwa idhini ya waathiriwa ili kuwabaini wanaodaiwa kuwa baba wa watoto hao.

Ripoti hiyo imefuatia agizo la Bunge mwaka jana kwa polisi kufanya uchunguzi huru baada ya Kamati ya Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni kubaini madai ya unyanyasaji wa kingono, matumizi mabaya ya mamlaka na ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na wanajeshi hao wa Uingereza.

Wakati huo huo wabunge wa Kenya wanataka makubaliano ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Uingereza yafanyiwe marekebisho ili kosa la mauaji lisikilizwe katika mahakama za Kenya, na BATUK iwajibike zaidi kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii.