Kwa nini Nguvu ya Marekani Inaelekea Ukingoni?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i140318-kwa_nini_nguvu_ya_marekani_inaelekea_ukingoni
Miongo mitatu baada ya operesheni ya "Desert Storm," mtazamo ndani ya duru za kimkakati za Marekani ni kwamba zama za nguvu na utawala usio na mpinzani wa Washington zimefikia ukingoni. Vita na Iran vimethibitisha kuwa mwenendo wa mabadiliko katika uwiano wa nguvu na kupungua kwa uwezo wa Marekani wa kuzuia vitisho (deterrence credibility) ndani ya mfumo wa dunia umeanza kushika kasi.
(last modified 2026-08-01T06:29:42+00:00 )
Aug 01, 2026 06:08 UTC
  • Kwa nini Nguvu ya Marekani Inaelekea Ukingoni?

Miongo mitatu baada ya operesheni ya "Desert Storm," mtazamo ndani ya duru za kimkakati za Marekani ni kwamba zama za nguvu na utawala usio na mpinzani wa Washington zimefikia ukingoni. Vita na Iran vimethibitisha kuwa mwenendo wa mabadiliko katika uwiano wa nguvu na kupungua kwa uwezo wa Marekani wa kuzuia vitisho (deterrence credibility) ndani ya mfumo wa dunia umeanza kushika kasi.

"Nguvu huwa na taathira kubwa zaidi pale panapokosekana haja ya kutumika nguvu yenyewe." Kwa miaka mingi, hali hii iliakisi nafasi ya Marekani katika mfumo wa dunia wa baada ya Vita Baridi. Ushindi wa haraka wa Marekani katika Vita vya Ghuba ya Uajemi vya mwaka 1991 uliimarisha mtazamo wa kimataifa kwamba Washington inaweza kuutwisha upande wowote hasimu matakwa yake ya kisiasa na kijeshi kwa gharama ndogo. Hata hivyo, miongo mitatu baadaye, swali la iwapo zama hizo zimefikia mwisho wake linaibuliwa hata ndani ya duru za kimkakati zenye hadhi ya juu zaidi nchini Marekani. Katika uchambuzi unaochochea fikra, jarida la Marekani la Foreign Affairs linaelezea hatua ya Marekani kuishambulia Iraq kama nukta muhimu ya mabadiliko katika mwelekeo wa uwiano wa nguvu duniani. Kwa mtazamo wa jarida hilo, mabadiliko haya yanaakisi mabadiliko katika kanuni za vita na kupungua kwa ubabe wa kijeshi wa Marekani katika kipindi cha baada ya Vita Baridi.

Si kushindwa kwa jeshi la Iraq ndiko kulifanya Operesheni ya Desert Storm (1991) kuwa tukio la kihistoria, bali vita hivyo viliimarisha dhana nne za msingi katika fikra za serikali, masoko, na wadau wa kimataifa. Dhana ya kwanza ilikuwa kwamba Marekani ingeweza kuamua kirahisi matokeo ya kijeshi, pili, ilikuwa na nguvu ya juu zaidi katika makabiliano yoyote ya kijeshi, tatu, ingedhamini kirahisi usalama wa njia za biashara ya kimataifa na ya nne ilidai kwamba kukabiliana na ubabe wa Marekani ni jambo hatari ambalo lingeandamana na gharama zisizo na dharura. Mtazamo huu potofu uliimarisha mfumo wa kambi moja yenye nguvu duniani na kuitwisha jamii ya kimataifa utawala wa kibabe wa Marekani.

Hata hivyo, vita vya sasa na Iran vimethibitisha wazi kwamba fikra hii haina maana tena. Mapungufu ya operesheni za kivita za Marekani katika eneo, changamoto za kukabiliana na mifumo hamishika, ndege zisizo na rubani za bei nafuu, na mitandao iliyotawanyika, yote hayo yanaonyesha kwamba teknolojia za kisasa zimevunja ukiritimba wa nguvu za kijeshi. Vita vinavyohusisha teknolojia za kisasa sio tena jambo linalohodhiwa na nchi chache zenye nguvu kubwa duniani. Nchi za eneo sasa zinaweza kutumia teknolojia zilizopo kwa ajili ya kuyasababishia gharama kubwa mataifa yenye nguvu duniani. Muhimu zaidi ni kwamba, mabadiliko haya hayahusiani tu na maendeleo ya kiteknolojia, bali ni mabadiliko ya kimsingi katika fikra nzima ya kuzuia uchokozi wa adui. Awali, ubora wa kijeshi wa Marekani ulikuwa chanzo cha imani kwa masoko ya dunia; makampuni ya usafirishaji, wawekezaji, ambapo serikali zilifanya shughuli zao zikiamini kuwa Washington ilikuwa na uwezo wa kudhamini usalama wa biashara ya kimataifa. Hata hivyo, imani hiyo inapopungua, madhara ya kiuchumi hujitokeza wazi, hata bila kuwepo vita kamili, yakianzia katika kupanda kwa gharama za bima kwa meli zinazobeba mafuta hadi kuvurugika kwa mifumo ya usambazaji bidhaa na kuongezeka hatari za kijiopolitiki.

Kama jarida la Foreign Affairs linavyobainisha, umuhimu wa taathira za mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran yanahusiana na suala hili hili. Kwa mtazamo wa jarida hilo, suala la msingi sio upande gani ulisababisha uharibifu mkubwa zaidi au ni maeneo mangapi ya kijeshi yaliyoharibiwa, bali swali la msingi ni kama Marekani bado inaweza kudhamini usalama kamili wa njia za kimkakati za kimataifa, kama ilivyokuwa katika miaka ya 1990. Kuulizwa swali kama hilo katika mojawapo ya machapisho yanayoongoza ya sera za kigeni nchini Marekani yenyewe ni ishara ya mabadiliko ya kifikra ndani ya duru za kimkakati za Magharibi. Wakati huo huo, kuenea kwa teknolojia za kibiashara kumebadilisha mienendo ya nguvu za jadi. Ndege zisizo na rubani, vitambuzi na mifumo ya juu ya mwongozo na mawasiliano si tena bidhaa za kipekee zinazohodhiwa na majengo makubwa ya kijeshi na viwanda. Utandawazi wa teknolojia umepunguza pengo kati ya mataifa makubwa na wachezaji wa kikanda, na kuwezesha kutolewa mashinikizo yasiyo na ulinganifu kwa kiwango kisicho cha kawaida. Kwa hivyo, ubora wa kiteknolojia hauendani tena na ushindi wa haraka na wa gharama nafuu. Bila shaka, mabadiliko haya hayamaanishi mwisho wa nguvu za Marekani, bali jambo la msingi zaidi ni kupungua kwa uwezo wa Washington wa kutumia nguvu hizo kufikia mafanikio ya kisiasa kwa gharama nafuu, faida ambayo ilikuwa nguzo muhimu ya mfumo wa dunia ya baada ya Vita Baridi.

Labda jambo muhimu zaidi linaloweza kufahamika kutokana na uchambuzi huu ni kwamba dunia imeingia katika hatua ambayo itibari ya nguvu ina umuhimu mkubwa zaidi kuliko ukubwa wake. Iwapo wadau wa kikanda, masoko ya nishati, na mashirika ya kimataifa yatahitimisha kuwa hakuna suala lolote kubwa katika Ghuba ya Uajemi linaloweza kushughulikiwa bila kuzingatia hali hizi mpya, basi uwiano wa nguvu utakuwa unabadilika taratibu. Kwa msingi huo, uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran hauwezi kuchukuliwa kama mgogoro wa kikanda tu. Kwa uchache, kwa mtazamo wa baadhi ya taasisi za uchambuzi na duru za kimkakati za Marekani, vita hivi vimekuwa jaribio la mfumo ulioibuka kufuatia kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti. Ikiwa mtazamo uliotolewa na jarida la Foreign Affairs ni sahihi, basi kilichoharibiwa katika vita hivi si ubora wa kijeshi wa Marekani pekee, bali ni udhibiti wa kisaikolojia na itibari ya kimkakati ya mfumo ambao ulikuwa umeeneza duniani ubabe wake wa kisiasa kwa zaidi ya miongo mitatu.