Umasikini waongezeka katika eneo la Ukanda wa Gaza, Palestina
Uchunguzi mpya uliofanywa unaonyesha kuwa, umasikini katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina umeongezeka katika kipindi cha muongo mmoja wa mzingiro wa utawala haramu wa Israel katika eneo hilo.
Jamal al-Khudri, mmoja wa wajumbe wa kamati ya wananchi ya kukabiliana na mzingiro wa Israel huko Gaza amesema kuwa, takribani wananchi milioni moja na nusu wa eneo la Ukanda wa Gaza wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Ameongeza kuwa, maelfu ya familia za Kipalestina huko Gaza zinaishi katika umasikini wa kupindukia. Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa kamati ya wananchi ya kukabiliana na mzingiro wa Israel huko Gaza ni kuwa, wastani wa kipato ni dola mbili kwa siku na kwamba, wananchi wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na matatizo chungu nzima kama kukatika huduma ya umeme, kuchafuka maji na kupatikana kwa shida huduma za afya na tiba.
Baadhi ya wananchi wa Ukanda wa Gaza wamewaambia waandishi wa habari kwamba,hali yao katika eneo hilo ni ya maafa. Kuongezeka umasikini katika eneo la Ukanda wa Gaza kumeifanya hali ya maisha katika eneo hilo izidi kuwa mbaya huku kukiwa hakuna matumaini yoyote ya kuboreka hali hiyo.
Tangu Januari mwaka 2006 na kufuatia ushindi wa harakati ya Hamas katika uchaguzi wa Bunge la Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel uliliwekea eneo la Ukanda wa Gaza mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa lengo la kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama.
Mzingiro huo unazuia kuingizwa katika eneo la Gaza bidhaa za mahitaji ya msingi zikiwemo za fueli, dawa na vifaa vya ujenzi.