Arab League nayo yataka Israel ipelekwe The Hague
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (The Arab League (AL) nayo imejiunga na harakati na taasisi nyingine za kikanda na kimataifa zilizolaani jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na imeutaka Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuanzisha uchunguzi kuhusu mauaji yaliyofanywa hivi karibuni na jeshi la Isrel dhidi ya raia wa Palestina.
Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo imesema: Inalaani vikali uihalifu wa wazi, unaofanyika kwa mpangilia maalumu na mkubwa dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina ambao unatambuliwa kuwa ni uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu kwa mujibu wa sherei za kimataifa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ahmad Aboul Gheit pia amelitaka Baraza la Usalama kuunda tume ya kimataifa ya kuchunguza ukatili na mauaji yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Itakumbukwa kuwa, Wapalestina wasiopungua 18 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,900 wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano ya siku ya ardhi yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yaliyoanza huko Palestina siku ya Ijumaa.
Baada ya mauaji hayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kulaani mauaji hayo. Baraza hilo limeshindwa hata kulaani kwa maneno tu jinai hiyo baada ya maafisa wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kukwamisha juhudi za kutolewa azimio au hata kulaani jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel.
Kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingereza, Jeremy Corbyn pia amesema: Mashambulizi ya askari wa Israel dhidi ya raia wa Palestina "yanashtua" huku seneta Bernie Sanders wa Marekani akiyataja kuwa ni "maafa na msiba".