Wakazi wa kisiwa cha Socotra Yemen waandamana kulalamikia uvamizi wa Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i44170-wakazi_wa_kisiwa_cha_socotra_yemen_waandamana_kulalamikia_uvamizi_wa_imarati
Raia wa Yemen wanaoishi katika kisiwa cha Socotra kwa siku ya pili mtawalia wamefanya maandamano kulalamikia uwepo wa wanajeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kisiwani humo.
(last modified 2026-02-03T09:36:48+00:00 )
May 07, 2018 15:00 UTC
  • Wakazi wa kisiwa cha Socotra Yemen waandamana kulalamikia uvamizi wa Imarati

Raia wa Yemen wanaoishi katika kisiwa cha Socotra kwa siku ya pili mtawalia wamefanya maandamano kulalamikia uwepo wa wanajeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kisiwani humo.

Abdallah bin Issa al Afrar, Mkuu wa Baraza la Umma la Wakazi wa Mikoa ya al Mahra na Socotra huko Yemen pia ametaka kuondoka wanajeshi wa Saudi Arabia na wa Imarati katika maeneo hayo na kusisitiza kuwa hakuna jambo linaloweza kuhalalisha kuwepo kijeshi Imarati na Saudia katika maeneo hayo mawili.

Wanajeshi wa Imarati wakiwa na vifaru vyao katika kisiwa cha Socotra, Yemen

Mkuu huyo wa Baraza Kuu la Wananchi katika mikoa hiyo miwili ya al Mahra na Socotra ameongeza kuwa, wakazi wa mikoa hiyo wanapinga kuwepo kijeshi nchi mbili za Saudia na Imarati. Wiki iliyopita kulichapishwa taarifa kuhusu hatua ya wanajeshi wa Imarati ya kuukalia kwa mabavu uwanja wa ndege katika kisiwa cha Socotra katika eneo moja liloloko baina ya Ghuba ya Aden na Bahari ya Hindi na kuvifukuza kisiwani hapo vikosi vyenye mfungamano na serikali iliyojiuzulu ya Yemen ya kibaraka wa Saudia. Wanajeshi wa Imarati walikikalia kwa mabavu kisiwa cha Socotra huko Yemen baada ya Saudi Arabia kutuma kamati ya kijeshi kwa ajili ya kutatua hitilafu zilizopo kati ya Imarati na serikali ya wakati huo ya Yemen. 

Hitilafu baina ya Imarati na Saudia zimepamba moto tangu mwaka mmoja uliopita kufuatia kitendo cha Rais aliyejiuzulu wa Yemen Abdu Rabbuh Mansour Hadi cha kumfukuza kazi Gavana wa Aden, Aidarus al Zubaidi aliyekuwa na mahusiano na Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Aidarus al Zubaidi (katikati), aliyekuwa gavana wa mkoa wa Aden nchini Yemen