Gaza na vita vingine vya majira ya joto kali?
Harakati za kichokozi za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ambazo zimekabiliwa na utayarifu mkubwa wa wapiganaji wa Batalioni ya Izzuddin Qassam, zimezidisha uwezekano wa kuanza vita vingine katika eneo hilo la Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Julai mwaka 2014 eneo la Ukanda wa Gaza lilishuhudia mashambulizi makali ya siku 51 ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Vita hivyo vilianza baada ya utawala huo ghasibu kudai kuwa Waisraeli watatu wametoweka katika Ukanda wa Gaza na kisha ukaituhumu harakati ya Hamas kuwa ndiyo iliyowateka nyara walowezi hao wa kizayuni. Hata hivyo baadaye ilidhihirika kwamba madai hayo hayakuwa ya kweli. Pamoja na hayo walowezi kadhaa wa Israel walimteka nyara kijana mmoja wa Palestina na kuteketeza mwili wake kwa moto baada ya kumuua shahidi. Baada ya ghasia za hapa na pale, baraza la mawaziri la Israel lilidhinisha mashambulizi na vita dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Wakati huo ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema kuwa, mashambulizi ya Israel mwaka 2014 huko Gaza ndiyo yaliyokuwa na uharibifu mkubwa zaidi na yaliyoua idadi kubwa ya raia tangu eneo hilo la ardhi ya Palestina lilipokaliwa kwa mabavu mwaka 1967. Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa: Katika mashambulizi ya siku 51 ya Israel dhidi ya Gaza Wapalestina wasiopungua 2,251 waliuawa shahidi na wengine 11,231 walijeruhiwa. Taarifa ya UN ilisisitiza kuwa asilimia 75 ya wahanga hao walikuwa raia wa kawaida wakiwemo wanawake na watoto wadogo na kwamba, asilimia 28 ya watu wa Gaza walipoteza makazi na nyumba zao katika vita na mashambulizi hayo.
Tangu mwaka 2008 hadi sasa Israel kwanza ilianzisha vita dhidi ya Gaza baada ya miaka minne katika mwaka 2012 na kisha ikaanzisha tena vita baada ya miaka miwili hapo mwaka 2014. Sasa imepita miaka minne tangu baada ya vita na mashambulizi ya Israel ya mwaka 2014 na kunaonekana ishara na daliliza vita vingine dhidi ya watu wa Gaza.
Utawala katili wa Israel umekuwa ukishambulia maeneo mbalimbali ya Gaza tangu watu wa eneo hilo walipoanza maandamano ya Haki ya Kurejea Nyumbani tarehe 30 mwezi Machi. Katika mfululizo huo huo Jumatano iliyopita wanaharakati watatu wa Batalioni ya Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas waliuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel huko mashariki mwa Gaza. Jinai hiyo imekabiliwa na jibu kali la Batalioni ya Izzuddin Qassam ambayo imesema waziwazi kwamba, damu za mashahidi hao hazitapotea hivihivi na zitachangia pakubwa katika historia ya mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.
Inaonekana kuwa katika kipindi cha sasa cha kukaribia kutimia miaka minne tangu baada ya mashambulizi ya siku 51 dhidi ya Gaza na mwaka wa 12 baada ya mashambulizi ya siku 33 ya Israel dhidi ya Hizbullah huko Lebanon, utawala katili wa Tel Aviv unapanga kuanzisha vita vingine katika majira ya joto ya mwaka huu wa 2018 huko katika Ukanda wa Gaza kwa matarajio ya kupunguza machungu na hasara za kushindwa katika msimu wa joto wa mwaka 2006 na 2014. Sambamba na kudhihiri dalili za vita na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, taasisi mbalimbali za kimataifa zimeendelea kutahadharisha kuhusu hali mbaya sana ya wakazi wa eneo hilo. Amjad Shawwa ambaye ni mratibu wa jumuiya zisizo za serikali za Palestina amesema hali ya Ukanda wa Gaza inafanana na baruti linalokaribia kulipuka na kwamba kila kitu katika eneo hilo kimevuka mstari wa tahadhari. Amesisitiza kuwa hadi sasa eneo la Gaza halijaondokana na athari mbaya za mashambulizi ya mwaka 2008 na 2014.
Kwa kutilia maanani hali hii inatupasa kusibiri na kuona je, jamii ya kimataifa itachukua hatua za kuzuia vita na mashambulizi mengine ya majira ya joto ya Israel dhidi ya watu wa Gaza, au utawala haramu wa Israel utatumia kimya na uzembe wa jamii ya kimataifa, misaada na himaya ya Donald Trump na unafiki na uzabazabina wa nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia kwa ajili ya kuanzisha vita vingine vyenye mauaji na uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza?