Mamluki 10 wa Imarati wauliwa kusini mashariki mwa Yemen
Duru za habari zimearifu kuwa mamluki wasiopungua kumi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wameuliwa kwenye mapigano kati ya wanamgambo wanaungwa mkono na nchi hiyo na wenyeji wa mkoa wa Shabwah unaopatikana kusini mashariki mwa Yemen.
Habari zinasema kuwa ndege za kivita za Imarati pia zilishiriki kwenye mapigano hayo. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa Imarati na wanamgambo wenye mfungamano na Abu Dhabi wanatekeleza hujuma huko kusini mwa Yemen ili kufanikisha malengo yao waliyoyakusudia ya kudhibiti maeneo yenye utajiri wa mafuta katika mikoa ya kusini mwa Yemen.
Hii ni katika halia ambayo, mnamo tarehe 5 Mei mwaka jana, Imarati ilikivamia na kukikalia kwa mabavu kisiwa cha kistratejia cha Socotra huko Yemen; hatua iliyoibua mvutano mkali kati ya Abu Dhabi na Abdu Rabbuh Mansour Hadi Rais wa Yemen aliyejiuzulu na muitifaki wa Saudi Arabia.

Kuungana na kushiriki pakubwa Imarati na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen kivitendo kumesababisha aina fulani ya ushindani baina ya nchi mbili hizo kuhusiana na maeneo yenye ushawishi huko Yemen. Uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na Saudi Arabia na Imarati huko Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa kuungwa mkono na Marekani kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wao Abdu Rabbuh Mansour Hadi; hadi sasa umesababisha kuuawa na kujeruhiwa makumi ya maelfu ya Wayemeni na kuifanya nchi hiyo ikabiliwe na uhaba wa chakula, dawa na maradhi mbalimbali.