B'Tselem: Jeshi la Israel huwaua kwa makusudi Wapalestina wanaoandamana Ghaza
Kituo cha Haki za Binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) kimeripoti kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni huwaua kwa makusudi na bila ya sababu raia wa Palestina wanaondamana katika maandamano yao ya amani ya haki ya kurejea katika mipaka ya Ghaza.
Kituo cha Haki za Binadamu cha B'Tselem kimeripoti kuwa mamia ya Wapalestina wameuliwa shahidi katika mipaka ya Ukanda wa Ghaza kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Kizayuni kinyume cha sheria na bila ya sababu yoyote. Kimeongeza kuwa, ufyatuaji risasi huo unatekelezwa na wanajeshi wa Kizayuni kwa idhini ya Mahakama Kuu ya utawala wa Kizayuni.
Kituo cha B'Tselem ambacho kinajishughulisha na upashaji taarifa kuhusu haki za binadamu huko Israel aidha kimeashiria kuwa duru nyingi rasmi za utawala wa Kizayuni zimekiri kwamba zinafahamu kuhusu kuuuliwa wafanya maandamano wengi wa Kipalestina katika mipaka ya Ghaza bila ya sababu wala halalisho lolote. Kituo cha B'Tselem kimeongeza kusema kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni haujali kivyovyote uhai wa wananchi wa Palestina na katika muda wa mwaka mmoja uliopita Wapalestina zaidi ya 300 waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi katika maandamano ya haki ya kurejea. Miongoni mwa waliouawa watoto walikuwa 37 na maelfu ya wafanya maandamano wengine walijeruhiwa.
Kituo cha B'Tselem aidha kimesisitiza kuwa duru rasmi za Israel zinafahamu vyema kuwa kuna tofauti kubwa kati ya yale yanayosemwa na maafisa wa Israel na ukweli wa mambo.