Makumi wauawa na mamia wajeruhiwa katika mapigano kusini mwa Yemen
(last modified Sun, 11 Aug 2019 14:47:39 GMT )
Aug 11, 2019 14:47 UTC
  • Makumi wauawa na mamia wajeruhiwa katika mapigano kusini mwa Yemen

Ofisi ya Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen imetangaza kuwa, makumi ya watu wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa kwenye mapigano ya karibuni katika mji wa Aden kusini mwa nchi hiyo.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa kuwa tangu tarehe 8 mwezi huu wa Agosti hadi hivi sasa, karibu watu 40 wameuawa na 260 wamejeruhiwa kwenye mapigano yanayoendelea katika mji wa Aden kati ya vikosi vya wapiganaji wanaoungwa mkono na Imarati na wale wa Saudi Arabia.

Muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia na Imarati sasa unapoigana vita vya niaba na kufanya mauaji na umwagaji damu  huko kusini mwa Yemen baada ya miaka minne ya kuishambulia nchi hiyo maskini ya Kiarabu.  

Mapigano katika mji wa Aden kati ya vikosi vinavyojulikana kwa jina la Ukanda wa Amani vya Baraza la Mpito la Kusini linalosaidiwa na  Imarati na wapiganaji watiifu kwa Abdrabbuh Mansur Hadi, rais aliyejiuzulu wa Yemen, ambao wanaungwa mkono na Saudi Arabia yamepamba moto tangu Agosti Mosi. 

Wapiganaji wanaosaidiwa na Imarati katika muda wa siku nne zilizopita wamedhibiti maeneo na kambi kadhaa za kijeshi, maeneo nyeti katika mji wa Aden na kuishilikilia ikulu ya al Maashiq ambayo ni makuu ya Mansur Hadi. leo pia ndege za kivita za Saudia zimeshambulia ikulu hiyo ya al Maashiq na eneo la Jebal Hadid mashariki mwa mji wa Aden. 

Mansour Hadi, Rais wa Yemen aliyejiuzulu