UAE yaanza kujitegenezea silaha, yawakasirisha wauzaji silaha wa Magharibi
Hatua ya Umoja wa Flame za Kiarabu (UAE) ya kuanza mpango wa kujiundia silaha zake inatazamiwa kuyakasirisha mashirika ya Kimagharibi ambayo huiuzia nchi hiyo silaha.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, UAE imeanzisha shirika kubwa la kiserikali ambalo limepewa jukumu la kuunda silaha za kisasa ambazo zitatumiwa na jeshi la nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Shirika hilo ambalo limepewa jina la EDGE, litajumuisha mashirika mengine madogo 25 ya serikali na linatazamiwa kuwaajiri wafanyakazi 12,000 huku pato lake la mwaka lilikadiriwa kuwa dola bilioni 5.
Katika Maonyesho ya Ndege ya Dubai yaliyofanyika mwezi uliopita, Jeshi la UAE lilitangaza kuwa shirika la EDGE limepewa kandarasi yenye thamani ya dola bilioni moja ya kuunda makombora ya kisasa ya kuelekezwa.

Kwa mujibu wa Reuters, sekta ya ulinzi ya UAE , kupitia shirika la EDGE, sasa inajiundia ndege zisizo na rubani au drone na pia silaha ndogo ndogo.
Inatazamiwa kuwa hatua hiyo ya UAE ya kuanza kujitengenezea zana za kivita itawakasirisha wauzaji wakubwa wa silaha duniani, yakiwemo mashirika ya Marekani.