Mahkama ya Yemen yamuhukumu kifo rais mtoro
Mahkama ya Jinai nchini Yemen imewahukumu adhabu ya kifo vibaraka wa Saudia akiwemo rais mtoro Abdrabbuh Mansur Hadi, Maeen Abdulmalik Saeed aliyekuwa waziri mkuu na Khalid Hussain Al Yamani, waziri wa mambo ya nje wa serikali iliyojiuzulu na kisha kutoroka nchi.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo iliyotolewa katika kikao cha mahkama hiyo ya jinai ikiongozwa na majaji Mujahid al-Amdi, Khalid Al-Mawardi, Ahmad Al-Qaiz na Khalid Omar, mbali na adhabu ya kifo dhidi ya Abdrabbuh Mansur Hadi, Maeen Abdulmalik Saeed na Khalid Hussain Al Yamani, mali zao zilizo ndani na nje ya nchi hiyo pia zitachukuliwa. Khalid Hussein Al Yamani amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mawasiliano haramu na utawala wa Kizayuni, kushirikiana na maadui, kufanya hadaa kwa kutumia jina la waziri wa mambo ya nje wa Yemen na hatua zingine zinazodhuru uhuru na haki ya kujitawala taifa la Yemen.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya Mahkama ya Jinai ya Yemen, Abdrabbuh Mansur Hadi na Maeen Abdulmalik Saeed wamehukumiwa kifo kutokana na kushirikiana na Al-Yamani katika makosa yake, kumchochea ili afanye ujasusi na kushirikina na maadui wa Yemen na pia kutoa amri kwa waziri mtoro wa mambo ya nje kushiriki katika mkutano wa mjini Warsaw, Poland na kughushi jina la rais na waziri mkuu wa Yemen. Itakumbukwa kuwa baada ya Abdrabbuh Mansur Hadi kujiuzulu urais hapo tarehe 22 Januari 2015 alivunja baraza la mawazidi lililokuwa likiongozwa na Khaled Bahah. Baada ya hatua hiyo tarehe 21 Februari 2015 alikimbia kutoka mji wa Sana'a na kuelekea mjini Aden na kisha mjini Riyadh, Saudia.